Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WAKULIMA wanaolima zao la kahawa wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, wameiomba serikali ya awamu ya tano hapa nchini, kuongeza kasi ya
usambazaji wa madawa yanayodhibiti zao hilo lisishambuliwe na wadudu
waharibifu, ili waweze kuzalisha kahawa kwa wingi na yenye ubora.
Aidha walieleza kuwa ugonjwa wa Chulebuni (CBD) ni ugonjwa
ambao huenea kwa kasi, ambapo mti wa kahawa ulioshambuliwa na ugonjwa huo
hupoteza asilimia 90 ya mavuno endapo mkulima hatazingatia namna ya kuzuia
ugonjwa huo.
Rai hiyo ilitolewa na wakulima hao kwenye maadhimisho ya siku
ya mkulima wa kahawa yaliyofanyika kijiji cha Mkinga kata ya Mapera wilayani
hapa, ambapo Taasisi ya utafiti wa zao la kahawa TaCRI wilayani humo imejiwekea
utaratibu wake kila mwaka wa maadhimisho hayo, ikilenga kuelimisha wakulima juu
ya kilimo bora cha zao la kahawa.
Siku hiyo ya mkulima wa kahawa, kumekuwa na utaratibu wa
kukutana pamoja na wenzao na kubadilishana uzoefu wa uzalishaji wa zao hilo,
kwa viwango vinavyokubalika katika soko la kimataifa.
Wakulima hao walieleza kuwa ugonjwa wa CBD huathiri matunda
ya kahawa, ambapo hushambulia mbuni wa kahawa hasa nyakati za masika pale maua
yanapochanua, punje zinapokuwa changa na zinapoelekea kuiva hivyo serikali
haina budi kuongeza kasi ya usambazaji wa pembejeo za kilimo cha zao hilo kwa
wakati.
Christian Mapunda ambaye ni mkulima wa kijiji cha Mkinga,
akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake alisema kuwa wakulima wa zao hilo ili
waweze kuepukana na usumbufu huo wa kahawa zao mashambani kushambuliwa na
wadudu waharibifu, ni vyema serikali ikaendelea na utaratibu wa kutoa ruzuku
kwenye miche bora ya kahawa aina ya vikonyo ambayo huzalishwa na TaCRI na
kusambazwa kwa wakulima.
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo, Ofisa kilimo na
mifugo wa wilaya ya Mbinga, Yohanes Nyoni aliwataka wakulima hao kuzingatia
kanuni za kilimo bora cha zao hilo kwa kushirikiana na maofisa kilimo waliopo
katika maeneo yao.
Nyoni alisema kuwa, wakulima hao wanapaswa pia kutumia
mitambo ya kisasa pale wanapokoboa kahawa mbivu mara baada ya kuichuma shambani,
ili iweze kuwa na ubora unaokubalika.
Vilevile Ofisa kilimo huyo alikemea biashara haramu ya magoma,
ambapo wafanyabiashara wajanja hupita kwa wakulima vijijini na kuwarubuni
wawauzie kahawa mbivu, kwa bei ndogo ikiwa bado shambani haijavunwa na kumfanya
mkulima mwisho wa siku aendelee kubaki kuwa maskini.
“Tushirikiane kuwadhibiti wafanyabiashara hawa, soko la
kahawa linahitaji kuimarisha ushirikiano lazima tujiunge kwenye vikundi au vyama
vya ushirika, tuache kufanya biashara ya kahawa mtu mmoja mmoja”, alisisitiza
Nyoni.
No comments:
Post a Comment