Na Mwandishi wetu,
Nyasa.
WAKULIMA wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamehimizwa kulipokea
zao jipya la kibiashara la Kokoa, kwa lengo la kuongeza kipato chao na kuimarisha
uchumi wa wilaya hiyo kwa ujumla.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mkuu wa wilaya Nyasa, Margaret Malenga
alipokuwa akizindua kilimo cha zao hilo wilayani humo, ambao ulifanyika
katika kijiji cha Songambele kata ya Kihagara.
Malenga alisema kuwa endapo watazingatia kilimo cha zao hilo,
wananchi hao wataweza kuongeza vipato vyao na kuwafanya kuachana na tabia ya kutegemea
shughuli za uvuvi pekee.
Licha ya kufanya uzinduzi huo, Mkuu huyo wa wilaya ya
Nyasa ameutaka uongozi wa vijiji kuhakikisha kwamba maeneo ya watu ambayo mpaka
sasa hayajaendelezwa kwa shughuli za kibinadamu, yaendeshwe shughuli za kilimo
cha zao la Kokoa.
Alisema kwamba, baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo
wamekumbatia maeneo makubwa yenye rutuba huku wengine wakihangaika maeneo ya
kufanyia kazi, jambo ambalo linasababisha wakose maeneo ya kuendeshea
shughuli za kiuchumi.
Maamuzi hayo yalifikia baada ya Mkuu huyo wa wilaya, kusomewa
taarifa na wananchi hao kuwa wengi wao wanalipenda zao hilo lakini changamoto kubwa
kwao, ni maeneo ya kufanyia shughuli za kilimo.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya ya Nyasa, Jabir Shekimweri alisema kuwa kwa upande wa wilaya hiyo wamejipanga
kikamilifu kuhakikisha kwamba, wananchi wanakuwa na maeneo ya kufanyia kilimo cha
zao hilo ambalo litakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi waishio mwambao mwa ziwa
Nyasa.
Shekimweri alisema pia wanajipanga namna ya kuangalia
uwezekano wa kuanzisha kilimo cha zao la Tangawizi, ambalo nalo halitumii
mbolea wala madawa ambayo huwafanya wakulima wengi kukatishwa tamaa ya kuendesha
shughuli za kilimo, kutokana na kukosa fedha za kununulia madawa au mbolea.
No comments:
Post a Comment