Na Kassian Nyandindi,
Njombe.
WAKAZI wa kijiji cha Mwilamba kata ya Kipengele wilaya ya
Wanging’ombe mkoani Njombe, wameitaka Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya hiyo kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi hao,
juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji vilivyopo kijijini hapo ambavyo ni tegemeo
kubwa kwa mkoa huo.
Aidha wamemuomba Mkuu wa wilaya hiyo, Asumpta Mshama kuacha
kutumia muda mwingi kukaa ofisini badala yake atembelee vyanzo hivyo ambapo walieleza
kuwa serikali ya wilaya, imevitelekeza kwa miaka mingi na kuwaachia wananchi
pekee waendelee kuvitunza.
Kauli hiyo ilitolewa na wakazi hao ambao waliomba majina yao
yasitajwe gazetini, walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari ambao
walitembelea kijijini hapo, kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo.
Wakizungumzia juu ya vyanzo hivyo, walisema kuwa kijiji hicho
kina zaidi ya vyanzo vya maji 26 ambavyo ndiyo huzalisha maji na kutumika
katika maeneo ya Njombe hivyo wanashangazwa na uongozi wa wilaya hiyo, kukaa
kimya bila kutembelea wananchi hao na kuunga mkono jitihada wanazozifanya katika
kuendelea kuimarisha vyanzo hivyo.
“Sisi wakazi wa kijiji hiki ndio tunaofanya kazi ya kutunza
vyanzo hivi, mara kwa mara tunapanda miti rafiki ya maji kwa lengo la
kuimarisha uoto wa asili usiweze kupotea, tumepeleka taarifa huko wilayani ili
wataalamu waweze kufika hapa kijijini kwetu watupatie elimu ya utunzaji wa
mazingira hatuja waona kwa muda mrefu na hii inaonesha kwamba hawataki
kutekeleza jambo hili”, walisema.
Lukemelo Mgaya ambaye ni diwani wa kata ya Kipengele,
alipohojiwa na waandishi wa habari alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo na
kueleza kwamba jambo hilo alilifikisha kwa viongozi husika ili liweze kufanyiwa
kazi, lakini anashangaa kuona hakuna utekelezaji uliofanyika.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe,
Meckedezeki Humbe alipoulizwa kuhusiana na kero hiyo alisema ofisi yake
haijawahi kupokea malalamiko hayo ya utunzaji wa vyanzo vya maji kwa wananchi
wa kijiji cha Mwilamba.
“Jambo hili kwangu ni jipya ndio kwanza mnaniambia, mimi
sijasikia lolote juu ya malalamiko haya subirini nikalifanyie kazi”, alisema
Humbe.
Mkuu wa wilaya hiyo, Asumta Mshama alipotakiwa kutolea
ufafanuzi kwamba pamoja na ofisi yake kuwa na taarifa juu ya suala hilo alisema
yeye hajawahi kupokea kero yoyote ya vyanzo hivyo, huku akiongeza kuwa mnamo
Machi 3 mwaka huu alitembelea kijiji hicho na wananchi hawakumwambia jambo
lolote lile kuhusiana na malalamiko hayo.
No comments:
Post a Comment