Yustina Chagaka, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani
Ruvuma imesema kwamba, katika mkoa huo watumishi wengi wa serikali wamekuwa
wakijihusisha na vitendo vya kushawishi na kupokea rushwa kutokana na kuwa
watovu wa maadili, katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi za kila siku.
Kufuatia hali hiyo, imeelezwa kuwa serikali imeazimia
kupambana na vitendo hivyo na kuwaasa watumishi hao, kuzingatia maadili ya kazi
zao na wananchi washiriki kikamilifu katika kutoa taarifa pale wanapoona au
kusikia kuna harufu ya vitendo vya rushwa.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Ruvuma, Yustina
Chagaka alipokuwa akitoa taarifa yake ya utendaji kazi kwa waandishi wa habari,
kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.
“Tumekuwa tukitekeleza matakwa ya sheria inayotuongoza kwa kuzingatia
majukumu makuu matatu, kuzuia rushwa, kuelimisha umma, kuchunguza tuhuma za
rushwa na kushtaki watuhumiwa wanaobainika kujihusisha na vitendo hivi kwa
mujibu wa sheria na majukumu haya yanatekelezwa kupitia madawati ya uchunguzi
na mashtaka, elimu kwa umma na dawati la utafiti”, alisema Chagaka.
Chagaka alifafanua kuwa katika kipindi hicho cha miezi
mitatu, ofisi yake imepokea taarifa 82 kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo
mbalimbali ambapo idara zinazoongoza kulalamikiwa kuwa ni mabaraza ya ardhi na
usuluhishi, mahakama, serikali za mitaa, ardhi, afya, elimu, kilimo na Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Alisema kuwa mpaka sasa idadi ya kesi zinazoendelea
Mahakamani zipo saba, huku akiongeza kuwa katika mkoa huo wilaya ya Mbinga
ndiyo inayoongoza kwa vitendo vya rushwa, na kwamba taasisi hiyo imewataka
wananchi kutoa ushirikiano wa karibu ili kuweza kudhibiti hali hiyo.
“Taasisi hii ikiwa ndiyo yenye dhamana ya kupambana na rushwa
hapa nchini, inawaasa watumishi wote wa serikali kuwatumikia wananchi kwa
uadilifu wakizingatia kanuni, taratibu na sheria zilizopo hivyo kwa yule atakayekamatwa
hakika tutamwajibisha”, alisema.
Mkuu huyo wa TAKUKURU alibainisha kuwa bado hawajafikia hatua
ya kuweza kujivuna kwamba, wanapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi
na mamlaka husika pale wanapohitaji kupata nyaraka wakati wanapofanya uchunguzi
wa jambo fulani.
Kadhalika akielezea mikakati ya mkoa huo, katika kumaliza
kero kwa wananchi hasa kwenye maeneo yanayoongoza kulalamikiwa kwa kushamiri
kwa vitendo vya rushwa alisema kuwa, taasisi hiyo inaendelea kufanya tafiti katika
idara mbalimbali za umma ambapo watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa
hatua za kisheria dhidi yao, wanajenga mahusiano madhubuti na wadau katika
kuhakikisha wanashiriki kikamilifu dhidi ya mapambano ya rushwa na kuelimisha
jamii kwa kufanya warsha zinazohusisha utoaji wa elimu husika.
No comments:
Post a Comment