Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho
amezindua rasmi Mamlaka ya mji wa Lusewa na kumuagiza Mkurugenzi wa
mamlaka pamoja na watumishi waliopelekwa kufanya kazi katika mamlaka hiyo,
kuhamia haraka huko ili waweze kwenda kuwahudumia na kutatua kero
zinazowakabili wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza
na mamia ya wananchi wa kata ya Lusewa, Msisima na Magazini katika
sherehe za uzinduzi wa mamlaka ya mji huo zilizofanyika katika
kijiji cha Lusewa wilayani hapa.
Chande Nalicho. |
Amewaagiza watumishi hao, kwenda kufanya kazi usiku na
mchana kwa kushirikiana na wananchi ili waweze kupata vigezo vya kuwa
halmashuri ya mji badala ya kuendelea kuwa mamlaka ya mji, jambo ambalo
linaweza kuwakosesha baadhi ya vitu muhimu vinavyotolewa na Wizara husika ya Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Alisema kuwa, mamlaka ya mji wa Lusewa ndiyo kwanza
inaanzishwa kwa lengo la serikali kusogeza huduma karibu na wananchi wake hivyo
ni jukumu sasa la watumishi hao kuhakikisha kwamba, wanajitolea muda wao
kufanya kazi na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao
ambao wana mategemeo makubwa baada ya serikali kuanzisha mamlaka hiyo.
Mamlaka ya mji wa Lusewa imeanzishwa kutoka halmashauri ya
wilaya ya Namtumbo, kutokana na umbali uliopo kutoka makao makuu ya
wilaya mjini Namtumbo hadi kata ya Lusewa ambapo ni umbali unaofikia zaidi
ya kilometa 110 kwa lengo la kusogeza karibu huduma kwa wananchi ikiwa ni mkakati
wa serikali ya awamu ya tano, kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kijamii
popote pale walipo ndani ya nchi.
Nalicho alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Astery Mwinuka
pamoja na timu yake kuhakikisha wanatekeleza majukumu husika ili waweze
kutekeleza maagizo ya serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwemo
agizo la Rais, Dkt. John Magufuli la kumaliza tatizo la upungufu
mkubwa wa madawati kwa shule za msingi na sekondari.
Pia ameitaka halmashauri mama ya wilaya ya
Namtumbo, kuwa karibu na kuitazama mamlaka hiyo mpya kwa ukaribu zaidi na kuipatia
kipaumbele ili watumishi waliopelekwa huko, kwenda kuanzisha mamlaka hiyo
waweze kutekeleza vyema majukumu yao ya kazi za kila siku.
Kuanzishwa kwa mamlaka ya mji huo kutachochea pia upatikanaji
wa maendeleo ya wananchi kwa haraka, na kwamba serikali itaendelea kutoa
ushirikiano kwa kuongeza wafanyakazi ambao ni wataalamu wa shughuli mbalimbali
kama vile katika nyanja ya kilimo na ufugaji.
Pamoja na mambo mengine Nalicho, alisikitishwa na
kushuka kwa kiwango cha elimu katika kata hiyo kwa kushika nafasi
ya mwisho kwenye matokeo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka uliopita 2015 ambapo
kati ya shule 10 zilizofanya vibaya, katika mitihani hiyo shule tano zimetoka
kata ya Lusewa.
No comments:
Post a Comment