Na Steven Augustino,
Tunduru.
DIWANI wa kata ya Tuwemacho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,
Khadija Mohamed amejikuta akiingia katika kashfa nzito baada ya kubainika
alikuwa amejiandikisha miongoni mwa kaya maskini, ambazo zimeingizwa kwenye
mradi wa uhaulishaji fedha unaotekelezwa na Mfuko wa Mendeleo ya Jamii (TASAF)
wilayani humo.
Khadija alibainika kuingizwa kwenye mpango huo, huku
akitambua kwamba anao uwezo wa kujimudu kimaisha, ambapo alibainika kufanya
hivyo baada ya TASAF wilayani hapa kufanya zoezi la kuhakiki majina ya walengwa
wanaostahili kupewa msaada wa fedha hizo ambao ni maskini hawajiwezi.
Sambamba na diwani huyo pia zoezi hilo limemng'oa Kaimu mtendaji
wa kijiji cha Nasya katika kata hiyo, Msamati Omary ambaye naye alijiandikisha
kuwa ni kati ya watu ambao wanastahili kupewa fedha hizo.
Kufuatia hali hiyo wengine walioondolewa katika mpango huo,
ni pamoja na Mwenyekiti wa kitongoji cha Malolo, aliyefahamika kwa jina la
Mohamed Malolo.
Pia Mwanajeshi mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ),
Mohamed Milanzi naye alikumbwa na kadhia hiyo wakati zoezi hilo linafanyika.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa utekelezaji wa
zoezi hilo, Mshauri na mfuatiliaji wa miradi ya Mfuko wa maendeleo ya
jamii wilaya ya Tunduru Christian Amani, alisema wanufaika hao
wameondolewa baada ya uchunguzi uliofanyika na kubaini hawana sifa za uwepo wao
katika mpango huo kwa sababu wanajiweza katika kumudu maisha yao ya kila siku.
“Tumefanya hivi kwa lengo la kuhakiki na kuwaondoa wajanja
wachache waliojipenyeza kiujanja ujanja katika mradi huu, ili wapate fedha za
kufanyia starehe za maisha yao”, alisema Amani.
Alisema inonesha kwamba, viongozi hao walijipenyeza kwa
kutumia mlango wa nyuma na wananchi wakawa wanashindwa kuwataja kwa kuwaogopa
huku akiwataka kutokana na kuenguliwa huko, waandike barua za kukata rufaa na
kuzipeleka TASAF ili zijadiliwe upya na kuzipitia kwa ajili ya kuondoa utata
endapo itabainika kama wameonewa.
Vilevile Amani alifafanua kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi
hilo, utafanyika utaratibu mpya wa kuingiza kaya zinazostahili kulingana na
sifa zilizoainishwa na mfuko huo ili kuweza kuepukana na matatizo kama hayo
yanayoweza kujitokeza tena hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment