Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MPANGO wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu katika Halmashauri ya wilaya ya Songea
mkoani Ruvuma, unatarajia kunufaisha kaya 5,016 zilizopo katika wilaya hiyo
ambazo zitapewa ajira za muda na kunufaika na mpango huo, utakaogharimu kiasi
cha shilingi milioni 865,260,000.
Ofisa ushauri na ufuatiliaji wa TASAF katika halmashauri hiyo,
Aniceth Kyaruzi, alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti
hili ofisini kwake mjini hapa.
Kyaruzi alisema kuwa halmashauri ya wilaya ya Songea,
imekwisha anza mchakato wake wa kuibua na kupanga miradi kwa ajili ya kutoa
ajira za muda katika vijiji 37 wilayani humo, ambavyo ni miongoni mwa vijiji 48
vinavyotekeleza mpango huo wa kunusuru kaya maskini.
Alifafanua kuwa miradi itakayopewa kipaumbele katika mfuko
huo, ni ile yenye manufaa ya muda mrefu kwa jamii hususan katika kukabiliana na
changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, mafuriko, ukame na upatikanaji wa
chakula.
Katika utekelezaji wa miradi hiyo, walengwa ni wale kaya maskini
zilizotambuliwa na kufanyiwa upembuzi yakinifu ambazo zinapokea ruzuku ya kila
mwezi ndio watakaokuwa wakifanya kazi hizo na kupewa ujira wa shilingi 2,300
kwa siku 60 katika mwaka.
Aliongeza kuwa mpaka sasa, kuanzia mwezi Septemba 2015 hadi Machi
2016, halmashauri ya wilaya ya Songea imekwisha toa ruzuku inayofikia
kiasi cha fedha za kitanzania, shilingi milioni 848 kwa kaya maskini 6,239
ambazo zinawalengwa wanaofikia 31,195.
Kwa upande wake Mratibu wa mpango huo katika halmashauri hiyo,
Hossana Ngunge alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa mpango huo wilayani humo
mafanikio mbalimbali yamepatikana ikiwemo kupambana na maadui watatu ambao ni
umaskini, ujinga, maradhi, kulipia gharama za matibabu, kuongezeka kwa kipato
katika kaya maskini pamoja na kupeleka watoto shule.
No comments:
Post a Comment