Na Steven Augustino,
Tunduru.
WATOA dawa kwa ajili ya kinga na tiba ya magonjwa
yaliyosahaulika, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ambao wanajiona kwamba
hawaendani na kasi ya utendaji kazi juu ya ugawaji wa dawa hizo, wametakiwa
kujitoa mapema kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Hayo yamejitokeza kufuatia uwepo wa taarifa kwa baadhi ya
wagawa dawa katika vijiji vya Nakapanya, Nalasi na vitongoji vyake wilayani
humo ambapo kati yao wametishia kutaka kugomea zoezi hilo wakishinikiza
waongezewe malipo ya ujira wa kufanya kazi hiyo.
Kaimu Katibu tawala wa wilaya ya Tunduru, Augustino Maneno alisema
hayo wakati alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo Chande Nalicho, kwenye
zoezi la kuwaongoza baadhi ya wananchi ambao walijitokeza katika uzinduzi wa
umezaji dawa hizo, uliofanyika hospitali ya wilaya iliyopo mjini hapa.
Magonjwa yaliyosahaulika na yale ambayo hayapewi kipaumbele
(NTD) ni pamoja na magonjwa ya matende, mabusha, ngiri maji na ndiyo ambayo
watu hupewa dawa ili yasiweze kuathiri afya zao.
Aidha katika uzinduzi huo Nalicho aliwataka wananchi wa wilaya
hiyo kujitokeza kwa wingi kumeza dawa hizo zitakazowasaidia pia kwa ajili ya
kinga na tiba ya magonjwa ya usubi, trakoma, kichocho na minyoo ya tumbo.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuondoa hofu na dhana
potofu kwamba, dawa hizo zinapunguza nguvu za kiume na kuleta madhara ya aina
mbalimbali.
Awali akisoma risala katika uzinduzi huo, Mratibu wa zoezi
hilo ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya macho hospitali ya wilaya ya Tunduru,
Zuhura Mshamu alisema tatizo linalochangia kuenea kwa magonjwa hayo linatokana
na uchafu wa mazingira, ikiwemo uwepo wa mito mingi yenye maji yaendayo kasi
hivyo kupelekea uwepo wa mbu aina ya Qullex ambaye husababisha ugonjwa wa
matende pamoja na inzi wadogo wanaoambukiza ugonjwa wa macho (Trakoma).
Zuhura alifafanua kuwa watu bilioni moja duniani,
wameathirika na magonjwa hayo na watu bilioni mbili wapo hatarini kupata
maambukizi ambapo kwa upande wa Tanzania, inakadiriwa kuwa zaidi ya watu
milioni 43 wapo mbioni kuambukizwa na watu milioni tano, wamekwisha
athiriwa na mojawapo ya magonjwa hayo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, naye Kaimu Mganga mkuu wa wilaya
hiyo, Dkt. Vitalis Lusasi alisema zoezi hilo wilayani humo litaendeshwa katika
zahanati na vituo vyote vya afya kwa kutoa dawa za kinga na tiba kwa magonjwa hayo
ili yasiweze kuleta madhara katika jamii hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment