Haya ni madaraja yanayolalamikiwa na Wananchi wa kijiji cha Mwilamba wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe, ambapo ujenzi wake umekuwa ni wa kusuasua. (Picha na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian
Nyandindi,
Njombe.
WANANCHI wa kijiji cha Mwilamba kilichopo katika kata ya
Kipengele wilaya ya Wanging’ombe mkoa wa Njombe, wameulalamikia uongozi wa
Halmashauri ya wilaya hiyo kwa kutochukua hatua za haraka kukamilisha ujenzi wa
madaraja mawili yaliyopo katika kijiji hicho, ambayo hivi sasa yanasababisha
washindwe kuendesha shughuli zao za maendeleo.
Aidha wananchi hao walisema kuwa kwa muda mrefu, madaraja
hayo ambayo yalianza kujengwa tangu mwezi Aprili mwaka jana hadi sasa ujenzi
wake unaonekana kusuasua, na hawajui ni lini yatakamilika ili huduma zao za
maendeleo ziweze kutekelezeka bila kuwepo usumbufu wa aina yoyote.
Walifafanua kuwa madaraja hayo, ambayo yapo katika mto
Nang’ano yanaunganisha kijiji cha Mwilamba hadi kwenye barabara kuu ya kutoka
Njombe mjini kwenda wilaya ya Makete.
Baadhi ya wananchi ambao waliomba majina yao yahifadhiwe,
waliwaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na hali hiyo ya ujenzi wa
madaraja hayo kutokamilika hasa kipindi hiki cha masika, mto huo hufurika maji
na wanashindwa kuvuka kwenda ng’ambo ya pili hasa pale wanapokuwa na wagonjwa
ambao wanapaswa kwenda nao kupata matibabu kwenye kituo cha afya cha Misheni
Kipengele ambacho kipo makao makuu ya kata hiyo.
Pia walieleza kuwa hata magari yanashindwa kwenda kwenye
kijiji hicho, na kulazimika kuishia karibu na yanapojengwa madaraja hayo ambayo
ujenzi wake umesimama, huwashusha abiria wanaokwenda kwenye kijiji cha Mwilamba
ambapo baadaye hulazimika kuvuka kwa kupita kwenye maji ya mto huo jambo ambalo
linaleta hofu juu ya maisha yao.
Wananchi hao walibainisha kuwa kijiji hicho ni maarufu kwa
kilimo cha viazi mviringo na upasuaji mbao na kwamba wafanyabiashara waliokuwa
wakifanya shughuli hizo, wanashindwa kwenda huko kutokana na madaraja hayo
kutokamilika ujenzi wake na kuwafanya wakulima wa viazi na wafanyabiashara wa
mbao kushindwa kuendesha shughuli zao ambazo zilikuwa zinawaletea kipato.
Kwa upande wake Afisa mtendaji wa kijiji cha Mwilamba, Jordan
Mtewele na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Mkabe Mbilinyi
walipozungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari walikiri kuwepo kwa
malalamiko hayo ambayo yamefikia hatua kuwa ni kero kubwa kwa wananchi, na
waliuomba uongozi wa halmashauri ya wilaya ya wanging’ombe kuchukua hatua za
haraka kabla madhara makubwa hayajatokea katika jamii kwa kumuhimiza mkandarasi
husika anayejenga madaraja hayo.
“Tatizo kubwa linalotusumbua kwenye madaraja haya, ni pale
panapotokea wagonjwa mahututi ambao wanalazimika kuwasafirisha kwenda kwenye
kituo cha afya cha misheni Kipengele au hospitali ya serikali ya wilaya ya
Njombe, tunashindwa kufika nao huko hasa pale mto huu ukiwa umefurika maji”,
alisema Mkabe Mbilinyi Mwenyekiti wa kijiji hicho.
Naye Diwani wa kata ya Kipendele, Lukemelo Mgaya alipohojiwa
alisema kuwa wananchi wa kijiji cha Mwilamba wanakabiliwa na changamoto nyingi
kutokana na madaraja kutokamilika ujenzi wake, na kwamba wamekuwa wakilazimika
kuwabeba wagonjwa kutoka kijijini hapo hadi ng’ambo ya mito hiyo kwa kutumia
machela kutoka na magari kushindwa kupita kwenye madaraja hayo.
Mgaya alifafanua kuwa kutoka kwenye kijiji hicho hadi makao
makuu ya kata ya Kipengele kuna umbali wa kilometa 15, hivyo kuna kila sababu
kwa serikali kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo ili wananchi waweze
kusafiri na kuendesha shughuli zao za kila siku, na kwamba tatizo hilo
anatarajia kulifikisha kwenye kikao cha Kamati ya uchumi na fedha ambacho
kitaketi Aprili 20 mwaka huu katika halmashauri hiyo.
Vilevile diwani huyo alimtaja Mkandarasi anajenga madaraja
katika mto Nang’ano kuwa ni wa kampuni ya ukandarasi ya Ajuwelo Masika iliyopo
Mafinga mkoani Njombe, ambapo ujenzi huo haujulikani utakwisha lini.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe,
Meckedezeki Humbe alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana kero hizo alisema ofisi
yake haijawahi kupata malalamiko yoyote juu ya ujenzi wa madaraja hayo.
“Ninyi ndio kwanza mnaniambia, mimi sijasikia lolote juu ya
malalamiko hayo subirini nikalifanyie kazi”, alisema Humbe.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya hiyo, Asumta Mshama alisema ujenzi
wa madaraja hayo unaoendelea kufanyika kwenye mto huo ulianza Septemba 9 mwaka
jana na kwamba ulitengewa fedha shilingi milioni 552,241,925 na Mkandarasi huyo
amekwisha lipwa kiasi cha fedha shilingi milioni 486,329,342 kwa hatua ya kazi
aliyoifanya katika mradi huo na kwamba ukamilishaji wa mradi unasubiri mvua
zipungue kunyesha ili aweze kuweka kifusi.
No comments:
Post a Comment