Baadhi ya wanabonanza la vijana wa Mbinga mkoani Ruvuma, la kuelimisha rika na usafi wa mazingira wakishiriki kuzoa taka katika eneo la soko la wakulima Mbinga mjini. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI waishio katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani
Ruvuma, wametakiwa kuzingatia masuala ya usafi kuanzia kwenye mazingira yao
wanayoishi majumbani kwao hadi katika maeneo wanayofanyia kazi au biashara, ili
waweze kuuweka mji huo katika hali ya usafi na kuepukana na magonjwa mbalimbali
ya mlipuko.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga
alipokuwa kwenye maadhimisho ya bonanza la vijana wa Mbinga la kuelimisha rika
na usafi wa mazingira, lililofanyika juzi katika uwanja wa taifa mjini hapa.
Bonaza hilo lilikuwa likienda sambamba na kauli mbiu isemayo;
zuia ngono zembe, mimba za utotoni, madawa ya kulevya na elimu inalipa.
Maadhimisho hayo yalifanyika kwa kuanza kufanya usafi katika
eneo la soko la wakulima lililopo mjini hapa kwa kuwashirikisha wananchi,
watumishi wa serikali na wale wanaotoka kwenye sekta binafsi.
Watoto Yatima wakiwa na Wanabonanza kituo cha Twiga Mbinga. |
Aidha waliweza kuwatembelea watoto yatima ambao wanalelewa
katika kituo cha kulea watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu
kinachofahamika kwa jina la Twiga, kilichopo kata ya Matarawe Mbinga mjini kwa
kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali kama vile sabuni za kuogea na kufulia,
daftari, kalamu, mafuta ya kupikia, sukari, pamoja na sare za shule.
Ngaga alisema kuwa kuna kila sababu katika jamii kuona
umuhimu wa kusaidia watoto hao, ili wasiweze kujiona wakiwa katika hali ya
kutengwa kwa kuwasomesha na hatimaye waweze kutimiza ndoto yao ya kuwa na
maisha bora.
Awali akitolea ufafanuzi juu ya maadhimisho hayo, Katibu wa
bonanza hilo Charles Kilili aliwaeleza waandishi wa habari kuwa msukumo wao
kama vijana ni kupeleka elimu kwa jamii, hasa kwa watoto wa kike waweze kuepukana
na mimba za utotoni na kwa wale wa kiume waachane na uvutaji wa madawa ya
kulevya kama vile bangi.
“Tunafanya haya mambo kwa kusisitiza masuala ya elimu husika
iweze kuwafikia kwa vitendo, tutahamasisha jamii uanzishaji na uundaji wa klabu
za kuelimisha watoto mashuleni juu ya kuachana na vitendo hivi, lengo ni kuwapa
elimu ya makuzi ikiwemo masuala ya uzazi wa mapango”, alisema Kilili.
Kilili alifafanua kuwa kwa kufanya hivyo, watakuwa wametimiza
azma yao ya kuwataka wanafunzi waepukane na hali hiyo kwa kujifunza juu ya
matendo mema wanayopaswa kuyafuata ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao darasani
na kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Naye Baraka Mwabulesi ambaye ni Mwenyekiti aliyekuwa
akiongoza maadhimisho ya bonanza hilo la uelimishaji rika na usafi wa
mazingira, alisema kwa upande wa kuweka mazingira wakati wote katika hali ya
usafi wanafanya hivyo kwa lengo la kuhamasisha jamii, kuwa na mazoea ya kufanya
usafi mara kwa mara katika maeneo yao.
Baraka alieleza kuwa jambo hilo wamelifanya kwa kumshirikisha
pia afisa afya wa halmashauri ya mji wa Mbinga, ili liweze kuwa endelevu kwa
wananchi wote wanaoishi katika mji huo.
Pamoja na mambo mengine wanabonanza walitoa vifaa vya
kufanyia usafi ambavyo ni vifaa vya kuhifadhia taka (dust bin), mifagio ya
kisasa, sabuni na ndoo za kunawia maji mara baada ya kufanya usafi, ambavyo
vilikabidhiwa kwa wafanyabiashara wa soko la wakulima lililopo mjini hapa.
No comments:
Post a Comment