Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
WANANCHI wanaoishi katika kijiji cha Milonji, kata
ya Lusewa wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wameaswa kupeleka kwa wingi watoto
wao shule ili waweze kupata elimu, ambayo itawasaidia kutoka katika hali ya
umaskini unaowakabili kwenye familia zao.
Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho alitoa rai hiyo juzi alipokuwa
akizungumza na wazazi na walezi pamoja na wananchi wa
kijiji hicho, katika mkutano wa hadhara wenye lengo la kutafuta
majawabu ya kukabiliana na changamoto zilizopo za watu kutotaka
kupeleka watoto wao shule, alipokuwa kwenye ziara ya siku mbili katika
kata ya Lusewa wilayani humo.
Chande Nalicho. |
Alisema kuwa, baadhi ya wazazi wamekuwa hawatendi haki kwa watoto
wao kwa kuwapa mahitaji ya msingi ikiwemo suala la kuwapatia elimu, jambo
ambalo ni sawa na ukatili mkubwa unaofanywa na wazazi kwa watoto
wao.
Alisisitiza kuwa kila mzazi anaowajibu wa kuhakikisha watoto alionao
watakapofikisha umri wa kwenda shule, ni lazima wawe wameripoti shule
ili wapate elimu ambayo ni urithi endelevu katika maisha yao ya kila
siku.
Mkuu huyo wa wilaya ya Namtumbo alifafanua kuwa hadi kufikia
mwishoni mwa mwezi uliopita, tayari shule ya msingi
Milonji imekwisha andikisha watoto 107 na imekuwa shule ya 8 ambayo
inaongoza kwa kuitikia wito wa Rais Dkt. John Magufuli ya elimu bure.
Katika hatua nyingine amewataka wananchi kushikiriana na
serikali, katika kupunguza tatizo kubwa la uhaba wa madawati linaloikabili
shule hiyo kwani mpaka sasa mahitaji halisi ni madawati 117, kwa hiyo
watumie rasilimali za misitu zilizopo katika maeneo yao kukabiliana na upungufu
huo mkubwa wa madawati.
Katika mpango huo, sio kila jambo lazima lifanywe na serikali
yao bali kila mmoja anapaswa kuhakikisha kwamba ni sehemu ya mafanikio katika
mpango huo ambao utasaidia, kuongeza kiwango cha ufaulu kwa vijana wao.
No comments:
Post a Comment