Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
WAKAGUZI wa elimu katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo
mkoani Ruvuma, wametakiwa kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yao
ya kazi ikiwemo kutembelea shule za msingi na sekondari mara kwa mara na
kuwachukulia hatua kali za kisheria, walimu wazembe ambao wanasababisha
wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao ikiwa ni mkakati wa
kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho
alipokuwa akizungumza na wakaguzi wa idara ya elimu ofisini kwake mjini hapa, ambapo
alikemea tabia ya wakaguzi kutumia muda mwingi kukaa ofisini na kuwaacha walimu
peke yao wakitumia muda mwingi wa kazi kufanya shughuli zao binafsi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba, hata tatizo la kushuka
kwa ufaulu katika wilaya ya Namtumbo linachangiwa na idara ya
ukaguzi kwa kushindwa kutembelea shule hizo kwa kuwafuatilia
utendaji kazi wa walimu hao.
Alisema kuwa baadhi ya wakaguzi ni kikwazo katika mkakati wa
wilaya hiyo, kuinua kiwango kiwango cha taaluma kwani wanatumia muda
wao kufanya shughuli zao binafsi na kushindwa kufuatilia maendeleo ya walimu,
ambao wanapata mishahara mikubwa mwishoni mwa mwezi huku baadhi yao wakionekana
wana randa randa mitaani kwa sababu zisizokuwa za lazima.
Mkuu huyo wa wilaya alikiri kwamba, idara hiyo inakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo suala la kutokuwa na magari ya kutosha ambayo
yangewezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa, kwani serikali inaendelea
kutafuta majawabu ya kukabiliana na kero hizo zilizopo katika idara hiyo ya
ukaguzi.
Nalicho ambaye pia kitaaluma ni mwalimu, alibainisha kuwa ni
aibu kuona wilaya hiyo bado inaendelea kushika nafasi ya mwisho kila
mwaka katika mitihani ya kitaifa, wakati kuna mazingira mazuri ya
walimu kufanya kazi zao hasa baada ya serikali kupitia halmashauri ya wilaya,
kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara ambazo zinaunganisha eneo moja kwenda
jingine.
No comments:
Post a Comment