Na Julius Konala,
Songea.
MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Benson Mpesya
amewaongoza baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Songea katika zoezi la
umezaji dawa kwa ajili ya kinga na tiba ya magonjwa yaliyosahaulika
na yale ambayo hayapewi kipaumbele (NTD) mjini hapa, ikiwemo ugonjwa wa matende.
Mpesya aliwaongoza wananchi hao katika uzinduzi uliofanyika
kwenye Zahanati ya gereza la Mahabusu mjini Songea, kwa kumeza dawa hizo za
kinga na tiba ya magonjwa ya usubi, mabusha, ngilimaji, trakoma, kichocho na
minyoo ya tumbo.
Akiwahutubia wananchi, wanafunzi wa shule ya msingi Majimaji,
walimu, askari magereza na watumishi wengine wa serikali waliojitokeza katika uzinduzi
huo, aliwataka kuondoa hofu na dhana potofu ya kwamba dawa hizo kwamba zina
madhara na kuwa na busha sio heshima katika jamii, bali ni matatizo makubwa.
Mkuu huyo wa wilaya aliwahimiza wananchi wengine, kujitokeza
kwa wingi katika kushiriki zoezi hilo linaloendelea mjini hapa pindi wataalamu
watakapokuwa wanazungukia maeneo mbalimbali, ikiwemo majumbani, shuleni na
katika vyuo.
Akizungumza katika zoezi hilo Daktari bingwa wa magonjwa ya macho
wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma, aliyejitambulisha kwa jina la Ngohi alifafanua
kuwa chanzo kikubwa kinachochangia kuenea kwa magonjwa hayo ni kutokana na
uchafu wa mazingira, wakiwemo mbu aina ya Currex ambaye husababisha ugonjwa wa
matende pamoja na inzi wadogo wanaoambukiza ugonjwa wa macho (Trakoma).
Kwa upande wake Mratibu wa magonjwa hayo yasiyopewa
kipaumbele katika Manispaa ya Songea, Broady Komba alisema kuwa inakadiriwa kuwa
watu bilioni moja duniani wameathirika na magonjwa hayo na watu bilioni mbili
wapo hatarini kupata maambukizi ambapo kwa upande wa Tanzania, inakadiriwa kuwa
zaidi ya watu milioni 43 wapo mbioni kuambukizwa na watu milioni tano,
wamekwisha athiriwa na mojawapo ya magonjwa hayo.
Komba alisema kuwa zoezi hilo litaendeshwa katika zahanati
zote za Manispaa ya Songea katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza wameanza
April 1 mwaka huu kwa kutoa dawa za kinga na tiba kwa magonjwa hya usubi, matende,
ngilimaji na minyoo huku akiongeza kuwa awamu ya pili zoezi hilo litafanyika
mwezi Agosti mwaka huu kwa kutoa dawa za kichocho kwa wanafunzi wa shule za
msingi huku akiitahadharisha jamii kuacha kuoga, kuogelea kwenye maji
yaliyotuama.
No comments:
Post a Comment