Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WANAWAKE ambao ni wajasiriamali katika Manispaa ya Songea
mkoani Ruvuma, wameiomba serikali kuwaandalia maeneo maalum ya kufanyia
shughuli zao za kila siku ili waweze kujiingizia kipato, badala ya kutumia
maeneo yasiokuwa rasmi ambayo yamekuwa yakiwasababishia adha kubwa wakati
wanapofanya biashara zao.
Baadhi ya wanawake hao walisema hayo hivi karibuni, walipokuwa
wakizungumza na mwandishi wa habari hizi huku wakieleza kuwa licha ya kujikita
na kutumia zaidi nguvu kubwa katika shughuli zao, changamoto kubwa wanayokabiliana
nayo hivi sasa ni kukosekana kwa mazingira rafiki ya kufanyia shuguli zao badala
yake hulazimika kutumia maeneo ambayo hayajatengwa kisheria jambo ambalo
huwasababishia usumbufu mkubwa, wa kufukuzwa na askari mgambo wa Manispaa hiyo.
Walisema kuwa, jambo hilo linawafanya kushindwa kusonga mbele
kimaendeleo katika maisha yao ya kila siku na hata kushiriki wakati
wa kuchangia shughuli mbalimbali za kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wajasirimali hao
Mary Mapunda anayejishughulisha na biashara ya kuuza matunda kando
kando ya soko kuu la Manispaa ya Songea, alisema kuwa licha ya Manispaa kuwaruhusu
kufunga baadhi ya barabara ili kupisha shughuli zao ziweze kufanyika, hata
hivyo bado maeneo hayo sio salama kwao kutokana na muda mchache wanaopewa
kufanya shughuli hizo za kibiashara.
Kwa mujibu wa Mapunda alifafanua kuwa muda wanaopewa ambao
ni kuanzia saa 12 jioni na kuendelea sio muda sahihi kwao, kwa
sababu wateja wengi tayari wanakuwa wamesharudi nyumbani na wanakuwa wamekwisha
nunua mahitaji yote ya nyumbani.
Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakijishughulisha na shughuli
mbalimbali za kuuza matunda, kama vile ndizi, embe na mbogamboga lakini
pindi wanapotafutwa na wateja wao hawapatikani kutokana na kukosekana kwa eneo
maalum, ambalo lingewakutanisha wajasirimali wanaouza bidhaa hizo kwa wateja
wao.
No comments:
Post a Comment