Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
SHIRIKA la Taifa
Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoani Ruvuma, limejipanga katika kuendelea kutoa elimu
kwa wananchi na watumishi wa serikali kwa kuhamasisha wajiunge na mifuko iliyoanzishwa
na shirika hilo, ili waweze kuepukana na ugumu wa maisha pale wanapofikia hatua
ya kustaafu utumishi wao serikalini.
Kauli hiyo
ilitolewa na Meneja wa shirika hilo mkoani humo, Dominic Mbwette alipokuwa
akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Songea huku akielezea shughuli
mbalimbali, zinazofanywa na shirika hilo.
Mbwette alisema
kuwa kuna baadhi ya wastaafu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu na
wengine hufariki dunia, kutokana na kukosa huduma za msingi katika maisha yao
ya kila siku hivyo ni vyema wajiunge na mfuko huo ili waweze kuondokana na
matatizo hayo yanayowakabili.
Kufuatia hali hiyo
amewaomba wananchi na wastaafu kujiunga na mifuko iliyoanzishwa na NSSF ili
waweze kunufaika na mafao mbalimbali, ikiwemo ya muda mrefu na muda mfupi.
Aliyataja mafao ya
muda mrefu yanayotolewa na shirika hilo kuwa ni Pensheni ya uzeeni, mafao ya
mkupuo maalum, Pensheni ya ulemavu na Pensheni ya urithi na kwamba aliendelea
kuelezea mafao ya muda mfupi kuwa ni mafao ya uzazi, mafao ya kuumia kazini
pamoja na mafao ya mazishi.
Meneja huyo
alizitaja changamoto zinazolikabili shirika hilo kuwa ni uelewa mdogo wa jamii,
kuhusiana na mifuko ya hifadhi jambo ambalo amedai kuwa shirika hilo
limejipanga katika kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuendelea kutoa elimu juu
ya umuhimu wa kujiunga na shirika hilo, ili kuweza kuongeza idadi ya wanachama.
Aidha alieleza
kuwa pamoja na changamoto hizo, lakini shirika hilo limeweza kupata mafanikio
kwa kutoa mikopo kwenye vyama vya akiba na mikopo (AMCOS) mbalimbali mkoani
humo, zikiwemo Ngaka, Mahilo, Pilikano, Ngima zote za wilaya ya Mbinga pamoja
na Wino Amcos iliyopo Madaba wilaya ya Songea vijijini.
No comments:
Post a Comment