Saturday, April 9, 2016

TUNDURU WASHUKURU KUPATIWA HUDUMA YA MATIBABU MACHO BURE

Wataalamu wa macho kutoka 'Bilal Muslim Mission Tanzania' wakitoa matibabu ya 'operation' kwa wagonjwa wa macho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.


Na Steven Augustino,
Tunduru.

WATU 4,292 wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamepatiwa  huduma ya matibabu ya macho kwa lengo la kuboresha afya zao na kuondokana na matatizo ya macho ambayo yalikuwa yakiwasumbua kwa muda mrefu.

Kati yao, watu 217 sawa na asilimia 5.3 ya wagonjwa wote waliopatiwa huduma hiyo walifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho, kansa ya macho, vikope na majipu yaliyokuwa yakiwasumbua katika macho yao huku wengine wakipewa miwani kwa wale wote waliobainika kuwa na mahitaji hayo.

Shirika la Bilal Musilm Mission Tanzania, ndilo lililotoa msaada wa matibabu hayo bure kwa watu hao, ambapo Mratibu wa matibabu hayo Dkt. Ain Sharif alisema hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya majumuisho ya utekelezaji wa zoezi hilo lililofanyika katika kambi ya kutolea huduma hiyo, iliyowekwa shule ya sekondari Frank Weston mjini hapa.


Akizungumzia taarifa ya kutofikiwa kwa idadi ya watu waliotarajiwa kupatiwa huduma hiyo, alisema ingawa taasisi yake imebanwa na ratiba ngumu ya kwenda kutoa huduma katika maeneo ya mikoa mingine alisema kuwa wanao mpango wa kuleta madaktari wengine wilayani humo mwishoni mwa mwezi huu Aprili, ili kuweza kumaliza utoaji wa huduma hiyo kwa watu ambao waliikosa.

Dkt. Sharif alieleza kuwa taasisi hiyo isiyo ya kiserikali, ilitarajia kutoa huduma kwa jumla ya watu 5,000 waishio wilayani Tunduru ambapo ina madaktari wake bingwa, waliobobea katika fani ya macho.

Kwa mujibu wa Dkt. Sharif alisema shirika hilo, ambalo liliambatana na madaktari 12 na kundi kubwa la wafanyakazi wa kujitolea walipanga kufanya upasuaji kwa watu zaidi ya 300 ambao walikuwa wakisumbuliwa na matatizo ya mtoto wa jicho na kwamba idadi hiyo haikufikiwa, kutokana na watu kutojitokeza kwa wingi.

Alisema huu ni mwaka wa 27 mfululizo kwa shirika hilo, kutoa huduma hizo katika maeneo mbalimbali hapa nchini na akatumia nafasi hiyo kupitia wataalamu hao kuwaomba wananchi wa mji wa Tunduru na wilaya kwa jumla, kujitokeza kupata huduma hiyo pindi watakapofika tena kwa ajili ya kutoa matibabu hayo bure.

Akitoa neno la shukrani kwa wataalamu hao, Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya hiyo Dkt. Mmari Zabron pamoja na kuwapongeza viongozi wa shirika hilo kwa uamuzi wa kupeleka huduma hiyo wilayani humo, alisema kuwa huduma hiyo imefika katika wakati unaohitajika kutokana na wananchi wengi walikuwa wakiishi katika upofu na hilo lilitokana na kushindwa kumudu gharama zake za matibabu.

Alisema wilaya hiyo ni miongoni mwa maeneo ambayo yanakabiliwa na magonjwa ambayo husababisha upofu yakiwemo usubi na trachoma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliojitokeza kupatiwa huduma hiyo ya matibabu ya macho, wakiwemo Shekhe mkuu wa wilaya ya Tunduru Waziri Chilakwechi, na wananchi wengine Salama Mwakajinga na Awetu Akukweti walisema wamefurahishwa kwa kupatiwa huduma hiyo, ambayo hapo awali walikuwa wakishindwa kumudu gharama zake kutokana na kukosa fedha.

No comments: