Na Julius Konala,
Songea.
KAMPUNI ya
usafirishaji abiria mikoani inayofahamika kwa jina maarufu la, Ilyana Company
Limited ya jijini Dar es salaam, imepanua huduma zake kwa kufungua ofisi zake
katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na kufanya idadi ya makampuni ya
usafirishaji mjini hapa, kuwa matatu.
Akizungumza na
gazeti hili ofisini kwake mjini Songea, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo,
Khalfan Kigwenembe alisema kuwa lengo la kufungua ofisi hiyo ni kwa ajili ya kuwasaidia
wananchi wa Manispaa ya Songea na mkoa kwa ujumla kusafiri kwa bei nafuu ambayo
imepangwa na serikali.
Kigwenembe ambaye
pia ni Diwani wa kata ya Namtumbo mjini, wilayani Namtumbo mkoani hapa, kupitia
tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema kuwa mabasi ya kampuni hiyo
yatafanya safari zake kuanzia Songea, Mbinga, Namtumbo hadi Dar es Salaam.
Amewataka
wafanyabiashara wengine wa usafirishaji wa abiria, kujitokeza kwa lengo
la kuwekeza kwenye wilaya zilizofikiwa na miundombinu ya barabara za lami,
na pia kutokana na kukua kwa mkoa huo na idadi ya watu kuongezeka.
“Naiomba Mamlaka
ya usafirishaji wa nchi kavu na majini SUMATRA hapa mkoani Ruvuma, kuzingatia
haki na usawa katika upangaji wa ratiba ya safari za magari ya abiria bila ya
kupendelea kampuni yeyote, kwa kuwa kila mfanyabiashara ana hiari ya kupeleka
gari yake mahali popote pale ilimradi anafuata sheria zilizowekwa ndani ya nchi”,
alisema Kigwenembe.
Kwa upande wake,
Fatuma Msusa mkazi wa maeneo ya Majengo katika Manispaa ya Songea alisema kuwa
kuongezeka kwa kampuni hiyo ya usafirishaji kutakuwa ukombozi mkubwa kwa
wananchi wa mkoa huo, akidai kuwa awali kulikuwa na adha kubwa ya usafiri pindi
shule zinapofungwa kutokana na magari hayo kusafirisha wanafunzi na kuwafanya
abiria wengine kusubiri zaidi ya siku tatu, kwa sababu ya uchache wa vyombo vya
usafiri uliopo.
Vilevile wananchi
wa Manispaa hiyo kwa nyakati tofauti hapa mkoani Ruvuma, wameishukuru na
kuipongeza kampuni hiyo kwa kuwasogezea huduma karibu na kuongeza kuwa uwepo wa
ushindani, maendeleo hupatikana kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment