Monday, April 25, 2016

MUVI RUVUMA YAWAUNGANISHA WAJASIRIAMALI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MRADI wa Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI) mkoani Ruvuma umeendesha kongamano, lililokutanisha taasisi za kifedha na wajasiriamali wadogo wadogo kwa lengo la kuwafanya waweze kutambua na kuchagua ni taasisi gani ya fedha watakayoweza kutumia katika kuendesha shughuli zao za kilimo, usindikaji na upatikanaji wa masoko ya kuuzia bidhaa zao wanazozalisha.

Jumla ya Wajasiriamali 150 ambao waliwakilisha wenzao 545 waliopo katika mnyororo wa thamani wa zao la mhogo, kutoka wilaya nne za mradi za Mbinga, Namtumbo, Songea Vijijini, na Nyasa.

Kongamano hilo ambalo lilifanyika juzi katika ukumbi wa chuo kikuu Huria tawi la Songea, lililenga kuwasaidia wajasiriamali hao waweze kuchagua ni   taasisi gani za fedha  wanazoweza kuzitumia katika shughuli zao za ujasiriamali wanazofanya kila siku na masoko katika zao la mhogo ambalo sasa lina soko kubwa ndani ya nchi na  nje ya nchi.


Taasisi zilizohudhuria na kutoa mada juu ya namna ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo kujikwamua kiuchumi kupitia huduma za kifedha ni; Benki ya Posta Tanzania, CRDB, NMB, na Benki ya Wananchi Mbinga (MCB).

Katika kongamano hilo, taasisi hizo za fedha ziliwasilisha mada juu ya aina ya mikopo, taratibu za kufuata kupata mikopo, riba inayotozwa, umuhimu wa kuweka akiba na taratibu za marejesho.

Wakielezea changamoto wanazokumbana nazo katika kupata mikopo, mjasiriamali Aidan Ngatunga kutoka wilaya ya Nyasa alisema changamoto kubwa kwao ni kiwango kikubwa cha riba kinachotozwa na benki, jambo ambalo linakuwa kikwazo katika kurejesha mkopo kwa wakati, hali hii inapelekea kunyanganywa mali ikiwemo nyumba, mashamba na vitu vya ndani.

Alisema kuwa taasisi za kifedha zimeanzishwa kwa lengo la kuwawezesha kuhifadhi akiba na kupata mikopo, ili mwisho wa siku waweze kuanzisha miradi ya kiuchumi ambayo itawasaidia  kupunguza umaskini walionao, lakini bado kuna ukiritimba mkubwa unaofanywa na watumishi wa benki na taasisi hizo ikiwemo kuwaomba rushwa wateja pale wanapohitaji mikopo.

Naye John Haulle mjasiriamali na mkulima wa mhogo kutoka wilaya ya Songea vijijini alisema, hivi sasa baadhi ya wateja wamekatishwa tamaa na taasisi hizo kwani zimegeuka adui mkubwa wa wateja tofauti na malengo ya kuwapunguzia mzigo wa umaskini wananchi hususan wale wenye kipato cha chini.

Alisisitiza kuwa suala la uaminifu kwa watumishi wa benki na vyama vya akiba na mikopo, umekuwa kwa kiasi kidogo jambo ambalo linawakatisha tamaa kuendelea kukopa fedha katika taasisi hizo.

Kadhalika wawakilishi kutoka benki za CRDB, NMB, Benki ya Wananchi Mbinga na Benki ya Posta Tanzania tawi la Songea waliwahakikishia wajasiriamali hao kwamba, taasisi zao zimejipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa wajasiriamali wa kipato cha chini wanapata fursa ya kukopa fedha katika taasisi zao hasa kwa vikundi kwa masharti nafuu.

Hata hivyo wawakilishi wa taasisi hizo, waliushukuru uongozi wa mradi wa MUVI kwa kuwaunganisha na wajasirimali hao kwani pamoja na kupata wateja wapya pia wameweza kufahamu juu ya changamoto mbalimbali, zinazowakabili wajasiriamali wadogo huku wakitoa wito kwa wajasiriamali kwenda kwenye taasisi hizo za kifedha kupata huduma za mikopo na kwamba watawapatia ushirikiano wa karibu, ili kuwawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuinua biashara zao.

No comments: