Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
VITENDO vya ushirikina ambavyo vilikuwa vikifanyika katika
shule ya sekondari Ngwilizi iliyopo kata ya Kitanda Halmashauri ya mji wa
Mbinga mkoani Ruvuma, vimedhibitiwa baada ya wazee wa kata hiyo kuketi pamoja
na kuzungumzia juu ya kumaliza kero hiyo.
Diwani wa kata hiyo, Zeno Mbunda alisema hayo alipokuwa
akizungumza na mwandishi wetu na kueleza kuwa muafaka huo ulifikiwa baada ya
kukubaliana na wazee hao kwamba, visiendelee kufanyika kwani vimekuwa
vikirudisha nyuma maendeleo ya walimu na wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo
na kata kwa ujumla.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga. |
“Wazee wamekwisha kaa vikao na kumaliza tatizo hili, kwa
makubaliano kwamba visiendelee kufanyika tena”, alisema Mbunda.
Awali hivi karibuni katika kikao kilichoketi Aprili 2 mwaka
huu, ilielezwa kuwa walimu na wanafunzi hao hufanyiwa vitendo vya hovyo nyakati
za usiku ambapo huteswa na wakati mwingine wakiwa wamelala, hujikuta wakiwa nje
ya nyumba zao wamevuliwa nguo walizovaa mwilini.
Pamoja na mambo mengine, akizungumzia juu ya mikakati ya kimaendeleo
aliyojiwekea katika kata hiyo Mbunda alisema kuwa wameunda kamati ya kuendeleza
zao la kahawa katika kata hiyo yenye lengo la kuwafanya wananchi wake, waweze
kushiriki kikamilifu katika kuendeleza kilimo cha zao hilo na kukuza uchumi
wao.
Alifafanua kuwa katika utekelezaji wa suala hilo, anahamasisha
pia uundaji wa vikundi vya ujasiriamali ambavyo kupitia Halmashauri ya mji wa
Mbinga vitasajiliwa na kuweza kwenda sambamba katika uzalishaji wa zao la
kahawa.
“Mpaka sasa katika kata yangu tuna vikundi 31ambavyo baadhi
yake vimesajiliwa na vingine bado vipo kwenye mchakato wa usajili, kata ya
Kitanda maeneo mengi yanafaa kwa uzalishaji wa zao la kahawa lengo langu la uhamasishaji
huu singependa wananchi wangu wajitikite katika uzalishaji wa mazao mengine
pekee, bali hata zao hili litawafanya wainue uchumi wao”, alisema.
Vilevile alieleza kuwa kilichobaki sasa ni kujenga
ushirikiano kati ya maofisa ugani waliopo katani humo na wakulima, ili kuweza
kufikia malengo husika waliyojiwekea.
Kadhalika alibainisha kuwa katika kufanikisha jambo hilo,
atafanya mikutano kuzunguka kata hiyo ambayo ina vijiji vitano ambavyo ni Lupilo,
Masimeli, Miembeni, Magangwala na Kitanda kwa lengo la kuhamasisha kilimo cha
zao la kahawa.
No comments:
Post a Comment