Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamsaka askari wake
wa kikosi cha kutuliza na kuzuia ghasia (FFU) mkoani humo mwenye namba F 5425
PC Emmanuel Nyagoli (35) kwa kosa la kutoroka jeshini, baada ya kukabiliwa na
tuhuma ya kugushi vyeti vya masomo wakati alipokuwa akijiunga na jeshi hilo
mwaka 2003.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa
Polisi mkoani humo Zubery Mwombeji alisema kuwa askari huyo alitoroka tangu Machi
16 mwaka huu, ilipobainika kwamba ametenda kosa hilo.
Mwombeji alisema kuwa PC Emmanuel, alikuwa ni askari wa
kikosi cha kutuliza na kuzuia ghasia na kwamba alipogundulika kuwa ana tatizo
hilo, ndipo alitoroka na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda huyo wa Polisi mkoani Ruvuma, ametoa rai kwa yeyote
atakayekuwa na taarifa zinazohusiana na askari huyo mahali alipo, atoe taarifa
katika kituo chochote cha Polisi kilichokuwa karibu naye.
Alifafanua kuwa askari huyo, alitoroka na kuacha vitambulisho
vyote vya kazi pamoja na sare kwenye nyumba aliyokuwa anaishi yeye na familia
yake na kwamba, hivi sasa hajulikani mahali aliko na Polisi inaendelea na
uchunguzi na endapo atakamatwa hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi
yake.
Katika hatua nyingine jeshi hilo la Polisi mkoani humo, limemtia
mbaroni Abdallah Juma mkazi wa Mjimwema katika Manispaa ya Songea kwa tuhuma za
kukutwa na gramu 500 za bangi alizokuwa amezihifadhi kwenye mfuko wa rambo.
Tukio hilo lilitokea Machi 28 mwaka huu, majira ya saa 5:40
asubuhi huko katika maeneo ya Matarawe mjini hapa.
Mtuhumiwa Juma alikamatwa na askari Polisi, ambao walikuwa
doria kwenye eneo hilo la Matarawe katika kibanda alichokuwa akifanyia biashara
ya kuuzia bangi, ambapo muda wowote kuanzia sasa mtuhumiwa atafikishwa
Mahakamani kujibu shtaka linalomkabili.
No comments:
Post a Comment