Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MHANDISI mkaguzi wa barabara na majengo Halmashauri ya mji wa
Mbinga mkoani Ruvuma, Jordan Kapinga amejikuta akiwa katika wakati mgumu
kufuatia Diwani wa kata ya Kitanda katika halmashauri hiyo, Zeno Mbunda kumtaka
atolee maelezo juu ya kwa nini ujenzi wa madaraja na barabara umejengwa kwa
kiwango cha chini ndani ya kata hiyo.
Hali hiyo ilifuatia baada ya Diwani huyo kuibua hoja hiyo,
katika kikao maalum cha Wenyeviti na wazee wa vijiji vya kata hiyo kilichoketi
kwenye ofisi za makao makuu ya kata ya Kitanda Aprili 2 mwaka huu, kwa lengo la
kujadili maendeleo ya kata hiyo na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wake.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. |
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunda alisema kuwa ujenzi wa
barabara na madaraja matatu ambao umefanywa katika kata hiyo haujashirikisha
wananchi na mkandarasi husika aliyepewa kazi hiyo hakuripoti kwa uongozi wa
kata hiyo jambo ambalo linawafanya wajenge shaka.
Kampuni ya Ndapa Interprises Corporation Company Limited
kutoka Dar es Salaam, alisema kuwa ndiyo iliyopewa kazi hiyo ambapo ujenzi wa
barabara na madaraja hayo umefanyika kwa kiwango cha chini.
Alifafanua kuwa daraja la mto Ruvuma, ambalo lilitengewa
fedha shilingi milioni 43,970,000 na ujenzi wake ulikuwa ni wa kuanzia mwezi wa
6 hadi wa 12 mwaka 2015 Kandarasi huyo cha kushangaza, ameanza kwa kujenga
nguzo tu na kutelekeza kazi hiyo.
Mbunda alibainisha kuwa alipofanya ufuatiliaji katika ofisi
za ujenzi halmashauri ya mji wa Mbinga, taarifa zinaonesha kuwa mkandarasi huyo
tayari alikwisha lipwa malipo ya awali shilingi milioni 13,194,000.
“Mnamo tarehe 11 mwezi Machi mwaka huu, nilikwenda kuwaona
wataalamu wa ujenzi walinihakikishia ujenzi wa daraja hili utafanyika lakini
mpaka sasa hakuna kazi iliyofanyika, na mhusika aliyepewa kazi ya ujenzi wa
miundombinu hii hajaripoti katika ofisi ya kata yangu tokea apewe kazi hizi ”,
alisema Kapinga.
Akizungumzia kwa upande wa ujenzi wa barabara katika kata
hiyo, alisema kuwa makalvati yaliyojengwa na kufukiwa barabarani yamebomoka
huku maeneo yaliyokuwa korofi ambayo yalikwanguliwa na greda, alililopitisha
wakati wa ujenzi huo yamebomoka hali ambayo inaonesha kwamba ujenzi wake
ulikuwa ni wa kiwango cha chini.
Kwa upande wao Wenyeviti na wazee hao kwa nyakati tofauti nao
waliibua hasira zao, wakiiomba serikali ichukue hatua ya kumkamata na kumshtaki
Mahakamani mkandarasi huyo ambaye ameshindwa kufanya kazi aliyopewa na
kusababisha kero kwa wananchi.
“Sisi tunataka tupate majibu ni lini huyu mtu amechukuliwa
hatua na Rais wetu John Magufuli apokee kilio chetu juu ya matatizo haya,
tunasema mkandarasi huyu ni mwizi tena ameingia katika kata yetu bila kutoa
taarifa mradi ameujenga chini ya kiwango”, alisema Castory Ndunguru Mwenyekiti
wa baraza la wazee kata ya Kitanda.
Vilevile Amon Ndunguru ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji cha
Masimeli katika kata hiyo, aliongeza kuwa dalili hizi zinadhihirisha wazi kuwa
mchakato wa tenda juu ya upatikanaji wa kazi hizo alizopewa mkandarasi
hazikufuatwa, ikiwemo wananchi waliopo katika eneo husika ambako mradi
unatekelezwa kwanza ilibidi washirikishwe ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya
lazima.
Mhandisi mkaguzi wa barabara na majengo Halmashauri ya mji wa
Mbinga, Jordan Kapinga aliposimama katika kikao hicho ili aweze kutolea
ufafanuzi juu ya malalamiko hayo kwanza alikiri juu ya diwani wa kata ya
Kitanda Zeno Mbunda kwenda kwenye ofisi za ujenzi za halmashauri hiyo,
kufuatilia kero hizo huku akiongeza kuwa yeye wakati miradi hiyo inajengwa
hakushirikishwa mchakato wake hivyo hawezi kutolea majibu sahihi, kwa sababu jambo
hilo lipo nje ya uwezo wake.
No comments:
Post a Comment