Na Steven Augustino,
Tunduru.
Yassin Raibu (31) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kazamoyo
wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30
jela baada ya kupatikana na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Adhabu hiyo ilitolewa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya
hiyo, Gladys Barthy baada ya Mahakama kujiridhisha na kutokuwa na mashaka dhidi
ya ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri, ambao ulipeleka mashahidi saba kwa
ajili ya kuthibitisha kosa hilo lililokuwa likimkabili.
Wakati huo Mahakama hiyo iliwaachilia huru watuhumiwa wengine
wawili waliokuwa wanadaiwa kushirikiana na Raibu katika tukio hilo na kupora
vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 7,175,000 mali ya Said
Khatib Yunusi, mkazi wa kijiji cha Lukumbule wilayani humo.
Walioachiliwa katika shauri hilo la jinai namba 44/2015 baada
ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na Mahakama hiyo na kuwaona kwamba hawana hatia
ni Barali Shamte (41) mkazi wa kijiji cha Mavuji wilayani Rufiji na Fadhili Mangambila
(43) mkazi wa kijiji cha Wenje wilayani Tunduru.
Awali akiwasomea shitaka hilo mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi
wa Polisi Inspekta Songelael Jwagu aliiambia Mahakama kuwa katika tukio hilo, watuhumiwa
hao wakiwa wanatumia bunduki aina ya SMG walimvamia Said Yunus na kumpora vitu
mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 1.7.
Katika shkata hilo Inspekta Jwagu, alisema kuwa katika tukio
hilo watuhumiwa hao waliiba fedha taslimu shilingi milioni 6,200,000, kamera
aina ya Sony yenye thamani ya shilingi 300,000, walichukua simu sita za mkononi
zenye thamani ya shilingi 425,000 pamoja na vocha za simu 2,500 za shilingi
1,250,000 majira ya saa 4.15 usiku Agosti 22 mwaka jana.
Akifafanua maelezo ya kosa hilo Inspekta Jwagu alisema
kuwa kwa kufanya tukio hilo watuhumiwa hao, walikiuka sheria namba 287 (a) ya
kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Baada ya Mahakama hiyo kumtia hatiani, Inspekta Jwagu
aliiomba Mahakama kuwapatia adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine ambao
wamekuwa na tabia kama hiyo.
Alisema taarifa zinaonesha kuwa mtuhumiwa huyo ni miongoni
mwa wahalifu sugu, ambaye alikwisha wahi kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo
cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana na hatia katika shauri la jinai namba
43/2015 baada ya kupatikana na kosa la kukutwa akiwa na bunduki aina ya SMG.
Raibu alipelekwa katika gereza la wilaya ya Tunduru na kuanza
kutumikia adhabu ya kifungo hicho kulingana na maelekezo yaliyotolewa na
Mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment