Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKULIMA wa mazao ya chakula na biashara wilayani Mbinga mkoa
wa Ruvuma, wametakiwa kujiunga uanachama na Umoja wa Chama Cha Wakulima Tanzania
(TFA) ili waweze kunufaika na fursa zilizopo, ikiwemo uzalishaji wa mazao yao
kwa ubora unaotakiwa.
Aidha imeelezwa kuwa ndani ya chama hicho, wakulima hao
wataweza kupata elimu juu ya kilimo bora cha kisasa, matumizi sahihi ya pembejeo
na kuingia mikataba na TFA ambayo baadaye itawawezesha kuwatafutia masoko ya
kuuza mazao yao ya chakula na biashara.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga alipokuwa
akizungumza kwenye maadhimisho ya ufunguzi wa duka la pembejeo za kilimo tawi
la TFA lililopo wilayani humo.
“Ndugu zangu dhana ya serikali ni kushirikiana na sekta
binafsi ili tuweze kuleta maendeleo hapa nchini, tuonyeshe utaalamu wetu katika
sekta ya kilimo tuongeze tija kwa wakulima kuwaunganisha kwenye vikundi na
kuwapatia elimu husika”, alisema Ngaga.
Pia Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga alisema kuwa, licha ya
wakulima wa wilaya hiyo kuzalisha mazao hayo kwa wingi lakini wanakabiliwa na tatizo
la kutokuwepo kwa maghala ya kutosha ya kuhifadhia mazao yao, hivyo alitoa
ushauri kwa chama hicho kuona uwezekano wa kuongeza ujenzi wa maghala hayo ili
kuweza kukidhi mahitaji husika wakati wa mavuno.
Vilevile alipongeza jitihada zilizofanywa na TFA kwa kufanya
uwekezaji wa duka la kuuzia pembejeo za kilimo katika wilaya hiyo, kwa kile
alichoeleza kuwa wilaya zilizopo nyanda za juu kusini ndiyo zinazofanya
uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara.
Awali akisoma taarifa ya maadhimisho juu ya ufunguzi wa duka
hilo, Mkurugenzi mtendaji wa TFA hapa nchini, Sarah Lyimo alieleza kwamba hiyo
ni taasisi kongwe ambayo ilianzishwa mwaka 1935 kwa lengo la kuwawezesha
wakulima wote pale ambapo kuna matawi yake, kusambaza na kuwafikishia pembejeo
na zana bora za kilimo zenye ubora wa hali ya juu kwa gharama nafuu.
Lyimo alifafanua kuwa taasisi hiyo hivi sasa ina matawi 12
yaliyopo katika mikoa ya Arusha, Moshi, Tanga, Dar es Salaam, Morogoro, Iringa,
Mafinga, Njombe, Mbeya, Mbozi, Babati na Karatu na ina jumla ya wanachama
4,800.
Alibainisha kuwa lengo ni kumuondolea mkulima matatizo ya
upatikanaji na matumizi hafifu ya pembejeo na kwamba, imejiwekea mikakati
kabambe ya kuwaelimisha wakulima wote hapa Tanzania juu ya kilimo bora na
chenye tija.
“Uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara hapa nchini,
unakabiliwa na changamoto nyingi na hili linasababishwa na huduma duni za ugani
na utafiti wakulima wengi wanalima bila kufuata kanuni za kilimo bora ikiwemo
kulima na kupanda kwa mstari, kupalilia kwa wakati, kuweka mbolea na madawa”,
alisema Lyimo.
Hata hivyo alisema urasimu uliopo katika upatikanaji wa
mikopo kwa wakulima na mikopo hiyo kuwa yenye riba kubwa, ni changamoto ambazo
wakulima wadogo na wakati zimekuwa zikiwatesa hivyo kupitia mtandao wa chama
hicho cha wakulima, serikali pamoja na wadau wengineo wa sekta ya kilimo
wataweza kuwafikia wakulima wengi kwa gharama ndogo na kwa haraka.
No comments:
Post a Comment