Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MJUMBE wa Kamati ya utendaji Taifa, Chama Cha Walimu Tanzania
(CWT) mkoani Ruvuma, Jema Mapunda ameipongeza serikali ya awamu ya tano ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa
kutoa elimu msingi bure, ambapo kupitia utekelezaji huo itaweza kuwapa fursa watoto
wa kike kupata elimu hiyo hadi sekondari kwa ufanisi mzuri.
Mapunda alisema hayo juzi, alipokuwa akifungua mafunzo ya
siku moja kwa walimu wanawake viongozi wa CWT mkoani hapa, yaliyofanyika mjini Songea.
Alisema kuwa familia nyingi awali zilikuwa zinasomesha watoto
wao kwa kuwapa kipaumbele watoto wa kiume, huku wakike wakibaki nyumbani kwa
kisingizio cha kukosa ada na michango mbalimbali jambo ambalo hivi sasa limekomeshwa
na Rais Dkt. Magufuli.
Alifafanua kuwa walimu wa kike, wanapaswa kuwa mfano mzuri kwenye
maeneo yao ya kazi kwa kuwahimiza wazazi wahakikishe kwamba, watoto
wao wanawapeleka shule bila kujali kuwa ni wa jinsia gani.
Vivilevile alieleza kuwa mafunzo hayo, yanawapa fursa ya
kupata elimu ya sheria ya kazi na ujasiriamali ili walimu hao wanawake toka
wanapokuwa kazini wawe wanafanya maandalizi, kujijenga kimaisha kabla ya
kustaafu na kwamba baadaye watakapofikia hatua ya kustaafu wasiweze kuwa
ombaomba au tegemezi.
Alisema elimu hiyo pia itawawezesha walimu hao, kupunguza
changamoto ya kuwa na madeni mengi yasiyokuwa ya lazima na kuwafanya washindwe
kutulia kwenye vituo vyao vya kazi na sio vinginevyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa dawati la jinsia na watoto mkoa
wa Ruvuma, Mrakibu msaidizi wa Polisi Anna Tembo alipozungumza katika mafunzo
hayo alisema kuwa ukatili wa kijinsia unaweza kuwa ni kipigo, ngono zisizokuwa
na utaratibu na kufanyiwa vitendo vya kinyama hivyo aliwataka walimu hao huko
waendako wakawe mabalozi wazuri katika maeneo yao ya kazi.
Anna alieleza kuwa vilevile walimu wanapaswa kupinga mfumo
kandamizi unaochangiwa kwa kiasi kikubwa kutoa lugha ambazo sio rafiki kwa
jamii, pamoja na mila na desturi kandamizi zipigwe vita.
Alibainisha kuwa walimu wanasaidia kwa kiasi kikubwa kwa
mambo mengi, hasa ikizingatiwa kuwa ndiyo wanaokaa kwa muda mrefu na watoto
shuleni tofauti na wazazi wao ambapo wanatakiwa kutoa elimu nzuri kwa wanafunzi
hasa wa kike ili waweze kuendana na maadili mema katika maisha yao,
yatakayowafanya waepukane na kudanganywa na matendo maovu.
No comments:
Post a Comment