Saturday, April 9, 2016

VITENDO VYA USHIRIKINA VYAWATESA WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI NGWILIZI

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa vitendo vya ushirikina ambavyo vinaendelea kufanyika katika shule ya sekondari Ngwilizi iliyopo kata ya Kitanda Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo ya walimu na wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo.

Diwani wa kata hiyo, Zeno Mbunda amekemea hali hiyo na kueleza kuwa walimu na wanafunzi hao hufanyiwa vitendo vya hovyo nyakati za usiku ambapo huteswa na wakati mwingine wakiwa wamelala, hujikuta wakiwa nje ya nyumba zao wamevuliwa nguo walizovaa mwilini.

Senyi Ngaga Mkuu wa wilaya ya Mbinga.
Mbunda alisema hayo alipokuwa kwenye kikao cha kujadili maendeleo ya kata ya Kitanda, kilichoshirikisha Wenyeviti wa vijiji na wazee ambacho kilifanyika juzi katika kata hiyo huku akiongeza kuwa hali hiyo inasababisha hata kwa watumishi wengine wa serikali waliopo huko, wanaishi kwa hofu wakiogopa mambo hayo ya ushirikina.

“Haya mambo wazee wenzangu hayafai inatupasa tuwe imara tubadilike, watoto nyakati za usiku pale shuleni hawalali wanateswa, masuala kama haya wanaoyafanya mnawafahamu, inabidi tuwaite tukae nao na kukemea hali hii kwa sababu wanaleta hofu kwa wengine na kushindwa kuishi kwa amani”, alisema Mbunda.


Naye Mwenyekiti wa baraza la wazee katika kata ya Kitanda, Castory Ndunguru alisema kuwa namna ya kudhibiti hali hiyo wanapaswa kupanga siku na kuitisha mkutano wa hadhara wa wananchi, ambapo siku hiyo itakuwa maalum kwa kupiga kura za siri zitakazoweza kuwabaini watu wenye kuendekeza vitendo hivyo vya ushirikina na kukemea hali hiyo isiweze kuendelea.

Ndunguru alifafanua kuwa walimu wa shule ya sekondari Ngwilizi, wakati mwingine wanapoamka asubuhi hujikuta wakiwa wamenyolewa nywele kichwani hivyo aliyataka mabaraza yote ya wazee katika vijiji vilivyopo kwenye kata hiyo, wafanye kazi ya kudhibiti hali hiyo kwa kuwanyoshea vidole wale wote wanaofanya matendo hayo.

Vilevile Menlufu Mbepera ambaye ni Katibu wa baraza la wazee kwenye kata hiyo, alibainisha kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikichangia kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya elimu na kata kwa ujumla.

Edward Pokela, Mwenyekiti wa kijiji cha Masimeli aliongeza kuwa wakati mwingine hata wananchi wa kata hiyo, wanapoamka asubuhi kwenye vyombo vyao vya kupikia huvikuta vikiwa vimepakwa damu.

Pamoja na mambo mengine alieleza kuwa, kufuatia kuwepo kwa hali hiyo kuna kila sababu kwa wale watu ambao wanafahamika kufanya vitendo hivyo vichafu wachukuliwe hatua, ikiwemo wapewe notisi ya kuhama ili waweze kuondoka katika kata hiyo.

No comments: