Na Kassian Nyandindi,
Songea.
USHAURI umetolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani
Ruvuma kwamba, Halmashauri za wilaya, mji na manispaa mkoani humo
kuanza utaratibu wa kutunga sheria maalum, itakayowabana watu wote wasiotaka
kujiunga na mfuko wa afya ya jamii na bima ya afya.
Abdiel Mkaro, ambaye ni Meneja wa NHIF Mkoani humo ametoa
ushauri huo alipokuwa akizungumza na gazeti hili juu ya mwamko mdogo wa
wananchi kujiunga na mfuko huo, kwa ajili ya kupata huduma bora za matibabu
pindi wanapougua.
Halmashauri hizo amezitaka kuhakikisha kwamba zinaongeza dawa
katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zake ili wanachama waliojiunga na
mfuko huo waweze kupata huduma ipasavyo pale wanapokwenda kupata
huduma kutokana na maradhi yanayowasumbua, ambapo baadhi ya maeneo wanachama
wamekuwa wakikosa dawa jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa wananchi
wengine kuogopa kujiunga na mpango huo.
Mkaro alisema kuwa endapo wataweka sheria ndogo ambazo zitamtaka
kila mwananchi kujiunga na mfuko huo, itasaidia kuongezeka kwa idadi ya
wanachama, hivyo kuwa na watu wengi wenye afya njema ambao watakuwa
na uwezo wa kufanya kazi za kujiletea maendeleo.
Alibainisha kuwa baadhi ya maeneo kumekuwa na mwamko mdogo wa
wananchi kujiunga na CHF na NHIF, kutokana na vituo vya kutolea matibabu
kutokuwa na dawa za kutosha hivyo kuwakatisha tamaa wanachama na wananchi
wengine ambao wanatamani kujiunga na mfuko huo.
Licha ya wataalam wa mfuko huo kujitahidi kutoa elimu
kwa wananchi na makundi mbalimbali ya kijamii, kama vile madiwani wa
halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma kuhusu umuhimu wao kujiunga, hata hivyo bado
kuna changamoto kubwa kwa makundi mengine ukiachilia
madiwani hao ambao wanabanwa moja kwa moja na utaratibu uliowekwa kutokana na
kazi zao.
Pia amewataka Wazazi na walezi kujiunga na huduma mpya ijulikanayo
kwa jina la Toto afya kadi, kwa watoto baada ya kuzaliwa
hadi miaka 18 kwa gharama ndogo ya shilingi 50,400 ambayo inatoa fursa
kwa mwanachama wa huduma hiyo, kupata matibabu kwa kipindi cha mwaka mzima.
Huduma ya Toto afya kadi, inalenga zaidi watoto
wadogo ambao wana umri huo wa kujiunga na NHIF kwa ajili ya kupata
matibabu bure wakati wote watakapougua badala ya mzazi kutembea umbali mrefu, kwa
lengo la kutafuta matibabu ya mtoto wake.
Pamoja na mambo mengine, alisisitiza kuwa wakati sasa umefika
kwa wazazi na walezi kutumia fursa hiyo adimu ya kujiunga na Toto afya kadi kwa
kile alichodai kuwa itaweza kumpunguzia gharama ya matibabu, pale
mtoto wake anapougua.
No comments:
Post a Comment