Thursday, April 21, 2016

WAJUMBE KAMATI YA SIASA WAFUNGA MAKUFULI OFISI ZA CCM NYASA

Na Kassian Nyandindi,

Nyasa.

WAJUMBE wa Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamefunga kwa makufuli Ofisi za chama hicho wilayani humo wakishinikiza kuwakataa Katibu wa wilaya hiyo, Greyson Mwengu kutokana na kudaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha zaidi ya shilingi milioni 50.

Aidha Katibu msaidizi wa CCM wa wilaya hiyo, Mussa Mwevi naye alikataliwa na kamati hiyo ya siasa kufuatia kutuhumiwa kushiriki kwa namna moja au nyingine kufanya ubadhirifu huo.

Tukio hilo lilitokea Machi 30 mwaka huu majira ya asubuhi, ambapo viongozi hao wa Chama cha mapinduzi wilayani humo wanadaiwa kutumia fedha hizo kinyume na taratibu ambazo zilitakiwa wakawalipe posho viongozi wa matawi, mabalozi na mawakala kipindi cha uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ya siasa ambao hawakutaka majina yao yatajwe kwa madai kuwa wao sio wasemaji wa chama, walisema hali hiyo ya ubadhirifu iligundulika mapema lakini kila walipokuwa wakihoji kupitia vikao vyao vya ndani walikuwa hawapati majibu sahihi.

Vilevile walisema kuwa walifikia hatua hiyo baada ya kuona kwamba, Katibu wa huyo wilaya ya Nyasa na msaidizi wake wamekuwa wakitoa maelezo yenye utata huku wahusika waliotakiwa kulipwa posho hizo, wakiendelea kudai na kuituhumu kamati ya siasa kuwa ndiyo iliyotafuna fedha hizo.

Walifafanua kuwa baada ya kufunga ofisi hizo makatibu hao, waliondoka kwenda makao makuu ya CCM mkoa yaliyopo Manispaa ya Songea wakisubiri hatma ya sakata hilo.

Pamoja na mambo mengine Katibu wa chama hicho wilaya ya Nyasa, Mwengu na mwenzake, Mwevi walipotafutwa ili waweze kutolea ufafanuzi juu ya tukio hilo walikataa kuzungumza na waandishi wa habari kwa madai kuwa wao sio wasemaji wa chama, huku wakisema atafutwe katibu wa chama hicho mkoa wa Ruvuma ili aweze kuzungumzia jambo hilo.

Jitihada za kumtafuta Katibu wa Chama cha mapinduzi mkoani humo, Verena Shumbusho zilifanikiwa ambapo alikiri kufungwa kwa ofisi hizo na kueleza kuwa Machi 31 mwaka huu, alikwenda Nyasa kutatua mgogoro huo ambao ulionekana kutishia usalama wa maisha ya viongozi hao.

Shumbusho aliongeza kuwa kutokana na hali halisi aliyoikuta huko, alilazimika kuwaamuru katibu wa wilaya hiyo na msaidizi wake kuondoka nao huku kamati ya hiyo siasa iliamriwa kufungua makufuli yaliyokuwa yamefungwa na kukaimishwa Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) wa wilaya hiyo, Anusiata Ngatunga mpaka hapo hali hiyo itakapo tengamaa.

Katibu huyo wa CCM mkoa wa Ruvuma, Shumbusho alipotakiwa kueleza ni kiasi gani cha fedha kimefanyiwa ubadhirifu na viongozi hao wa wilaya ya Nyasa alikataa kutoa ufafanuzi na kusema kuwa, huo ni mkakati wa ndani ya chama hawezi kueleza ni kiasi gani cha fedha kilichokwapuliwa na kufanyiwa matumizi kinyume na taratibu.

No comments: