Na Julius Konala,
Namtumbo.
KITUO cha afya Msindo, kilichopo katika Halmashauri ya wilaya
ya Namtumbo mkoani Ruvuma, kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
ukosefu wa maji na umeme jambo ambalo linakwamisha utendaji kazi kwa watumishi
waliopo katika kituo hicho.
Jimmy Runje ambaye ni Mganga mkuu wa kituo hicho alieleza
kuwa wanapohitaji huduma ya maji, hulazimika kuyafuata umbali mrefu na
kuwafanya kuwa katika wakati mgumu hasa pale wanapofikia hatua ya kufua mashuka
ya kulalia wagonjwa.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na mganga mkuu huyo alipokuwa
akizungumza na mwandishi wetu, ambaye alitembelea kituo hicho kwa ajili ya
kujionea changamoto mbalimbali.
Akizungumzia juu ya changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme
kituoni hapo, alisema hali hiyo inasababisha shughuli za upimaji kitengo
cha maabara zishindwe kufanyika ipasavyo, kutokana na mashine wanayotumia mionzi
ya jua hususan nyakati za usiku kushindwa kufanya kazi vizuri.
Akizungumza na gazeti hili mzee mmoja aliyejitambulisha kwa
jina la, Folkward Sanga aliiomba serikali kumaliza tatizo la upatikanaji wa
dawa hasa katika vituo vya afya, ambavyo vinalaza wagonjwa.
Sanga aliongeza kuwa katika vituo hivyo kumekuwa na tatizo la
ukosefu wa nyumba za kuishi watumishi, hivyo kuna kila sababu kwa serikali
kuchukua hatua ya kunusuru hali hiyo ikiwemo kuwajengea nyumba ili waweze
kuondokana na adha ya kupanga uraiani.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya
ya Namtumbo Ally Mpenye, amekiri kuwepo kwa upungufu wa madawa alisema kuwa atazungumza
na wizara husika kuangalia uwezekano wa kuongeza kiwango cha dawa hizo.
Alisema kuwa halmashauri hiyo, ipo pia katika mpango wa
kutatua changamoto nyingine za ukosefu wa nyumba za kuishi waganga katika
zahanati na vituo vya afya, vilivyopo wilayani humo.
Kituo cha afya cha Msindo kinahudumia wananchi wa vijiji vinne
ambavyo ni Mtakanini, Lumecha, Nambehe na Msindo ambapo kituo hicho kinauwezo
wa kulaza wagonjwa 20 hadi 25 kwa siku.
No comments:
Post a Comment