Na Steven Augustino,
Shirika la Bilal Musilm Mission, ndilo lililotoa huduma hiyo ambapo Dkt. Ain Sharif ambaye ni mratibu wa huduma hiyo alisema kuwa ilikuwa ikitolewa hivi karibuni katika shule ya sekondari, Frank Weston iliyopo mjini hapa.
Tunduru.
ZAIDI ya watu 5,000 waishio wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamenufaika
na huduma ya matibabu ya macho iliyotolewa wilayani humo kwa lengo la kuboresha
afya zao, kutokana na wengi wao kusumbuliwa na matatizo mbalimbali ya magonjwa
ya macho.
Shirika la Bilal Musilm Mission, ndilo lililotoa huduma hiyo ambapo Dkt. Ain Sharif ambaye ni mratibu wa huduma hiyo alisema kuwa ilikuwa ikitolewa hivi karibuni katika shule ya sekondari, Frank Weston iliyopo mjini hapa.
Sharif alisema kuwa jumla ya madaktari 12 wakiwemo madaktari
bingwa watano wa huduma za macho walishiriki katika zoezi hilo, ambalo lilidumu
kwa muda wa siku nne.
Alisema wataalamu hao walitoa huduma ya kupima macho, kutoa
dawa, kufanya upasuaji wa kutoa mtoto wa jicho na kutoa miwani kwa watu waliobainika
kuwa na mahitaji hayo.
Kwa mujibu wa Dkt. Sharif pamoja huduma hizo kutolewa, pia shirika
hilo ambalo liliambatana na madaktari hao na kundi kubwa la wafanyakazi wa
kujitolea walifanya upasuaji kwa watu zaidi ya 300, ambao walikuwa
wakisumbuliwa na matatizo ya mtoto wa jicho.
Alisema katika utekelezaji wa zoezi hilo, walitoa huduma hiyo
pamoja na waliohitaji kupatiwa dawa za kutibu matatizo ya macho yao, huku
huduma hizo zikitolewa bure bila malipo yoyote.
Ni mwaka wa 27 mfululizo kwa shirika hilo kutoa huduma
hizo, katika maeneo mbalimbali hapa
nchini.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dkt. Mmari
Zabron pamoja na kuwapongeza viongozi wa shirika hilo kwa uamuzi wa kupeleka
huduma hiyo wilayani humo, aliwataka wananchi wenye matatizo mbalimbali ya
kiafya kuendelea kujitokeza kwa wingi ili waweze kupatiwa huduma.
Alisema wilaya hiyo ina uhitaji mkubwa wa huduma za macho na
kwamba watu wengi wamekuwa wakiishi katika upofu, kutokana na kushindwa kumudu
gharama zake ambazo hutolewa katika hospitali za kulipia.
Wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na
magonjwa ambayo husababisha upofu yakiwemo usubi na trachoma.
No comments:
Post a Comment