Na Kassian Nyandindi,
Songea.
IMEELEZWA kwamba serikali hapa nchini, itahakikisha
inaboresha na kuimarisha mitambo yake ya kurusha matangazo katika mkoa wa
Ruvuma, kupitia redio ya Taifa (TBC) kituo cha Songea ili kuifanya wilaya ya
Nyasa na Namtumbo mkoani humo, ziweze kufikiwa na matangazo mbalimbali
yanayorushwa na kituo hicho kwa ufanisi mzuri.
Kauli hiyo ya serikali inafuatia baada ya wananchi wa mkoa
huo, kulalamika kwa muda mrefu kuwa redio hiyo ya taifa matangazo yake
hayawafikii katika wilaya hizo na badala yake muda mwingi wanapofungua redio
zao, husikia matangazo ya kutoka katika redio zilizopo nchi ya Malawi na
Msumbiji.
Naibu Waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Anastazia
Wambura alisema hayo hivi karibuni mjini hapa alipokuwa kwenye kikao maalum akizungumza
na waandishi wa habari, pamoja na baadhi ya watumishi wa serikali mkoani humo.
Wambura alikuwa katika ziara yake ya kikazi ambapo alifafanua
kuwa, wamejiwekea mikakati kwamba katika kipindi cha utawala wa serikali hii ya
awamu ya tano lazima TBC iboreshe mitambo yake ili wananchi katika maeneo yote
hapa nchini, hususan kwa yale yaliyopo pembezoni mwa nchi yanawafikia matangazo
hayo ipasavyo.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alizitaka Halmashauri za
wilaya kutenga bajeti ya kutosha katika sekta ya michezo, ambayo itaweza kuleta
ufanisi mzuri kwa utekelezaji wa mambo mbali mbali.
“Licha ya kutenga bajeti naagiza pia katika michoro yenu ya
mipango miji, hakikisheni mnatenga na viwanja vya michezo ambavyo wananchi
watakuwa wanapata fursa ya kupumzika na kustarehe baada ya kufanya shughuli zao
za kimaendeleo”, alisisitiza.
Awali akisoma taarifa fupi ya maendeleo ya michezo mkoani
Ruvuma, Ofisa michezo wa mkoa huo Hassan Katuli alieleza kuwa kuna upungufu
mkubwa wataalamu wa michezo na viwanja vyake.
Katuli aliongeza kwa kuiomba Wizara kuharakisha zoezi la
kuajiri wataalamu hao kwenye halmashauri, ili waweze kutoa mafunzo kwa vijana
mashuleni katika sekta hiyo ya michezo.
No comments:
Post a Comment