Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
MKURUGENZI mtendaji wa Mamlaka ya mji wa Lusewa, wilayani
Namtumbo mkoa wa Ruvuma Astery Mwinuka, amepiga marufuku tabia ya vijana
kufanya maandamano yasiyokuwa ya lazima pindi wanapodai haki zao, badala yake wafuate
sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwemo kutumia Ofisi ya Mamlaka hiyo
katika kutafuta majawabu ya kero zao mbalimbali zinazowakabili.
Mwinuka alitoa onyo hilo, mara baada ya kukabidhiwa
rasmi majengo yatakayotumika kama Ofisi za Mamlaka ya mji wa
Lusewa katika sherehe fupi iliyofanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na
wananchi wa kata tatu za Lusewa, Msisima na Magazini ambazo kwa pamoja zimeunda
mamlaka hiyo.
Alisema kuwa tayari serikali imesikiliza kilio chao
kwa kuanzisha mamlaka ya mji huo ambayo itakuwa na dhamana ya kusimamia
shughuli zote za maendeleo, kutatua kero na kukabiliana na changamoto
mbalimbali, hivyo ni vyema wananchi wakawa na utaratibu wa kupeleka kero zao
katika ofisi hizo badala ya kuanzisha migogoro isiyokuwa na tija kwao.
“Tumepata mamlaka ya mji kamili hapa Lusewa, natoa onyo kali
kuanzia sasa hakuna tena maandamano ambayo yatawapotezea muda wenu wa kufanya
kazi kama kuna tatizo tumieni ofisi za mamlaka na sio kukimbilia kwa mkuu
wa wilaya, mtapoteza muda wenu wa kufanya kazi na wengine mtajikuta mkiishia mikononi
mwa vyombo vya dola”, alisema Mwinuka.
Aidha amepiga marufuku, vijana kutumia saa za kazi kucheza mchezo
wa Pool au kuzungumzia mambo ya siasa, badala yake amewataka watumie muda wao
katika kufanya kazi za uzalishaji mali hususani kilimo ambacho kina nafasi
kubwa ya kumaliza tatizo la umaskini katika familia zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya
Namtumbo, Danny Nyambo amewataka wakazi wa kata ya Lusewa na maeneo jirani
kuhakikisha kwamba wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa watumishi hao,
ili mamlaka hiyo iweze kutekeleza na kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.
Nyambo alibainisha kuwa kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ni jambo
la faraja kwa wananchi wote wa wilaya ya Namtumbo, kwa kuwa itasaidia kuharakisha
upatikanaji wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, halmashauri na mkoa wa Ruvuma kwa
ujumla.
No comments:
Post a Comment