Na Steven
Augustino,
Tunduru.
WAFUNGWA wawili ambao walikuwa wakitumikia kifungo katika gereza
la kilimo na mifugo Majimaji, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wamefariki dunia papo
hapo baada ya kupigwa na radi.
Sambamba na vifo hivyo, pia watatu walijeruhiwa baada ya
kupigwa na radi hiyo na kukimbizwa hospitali ya wilaya hiyo, kwa ajili ya
matibabu zaidi ambako wamelazwa na hali zao bado ni mbaya.
Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea
majira ya jioni Marchi 18 mwaka huu, wakati wafungwa hao wakiwa wamekwisha
fungiwa gerezani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji
amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa ni mipango ya Mungu, hivyo
hakuna wa kumlaumu.
Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni mfungwa namba 15/2016
Hassan Mtewa (32) mkazi wa kijjiji cha Nandembo wilayani humo, ambaye alikuwa
anatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kupatikana na hatia katika
kosa la wizi wa kuku.
Kamanda Mwombeji alimtaja mwingine aliyefariki kuwa ni mfungwa
namba 29/2015 Issa Daudi (40) mzaliwa wa wilaya ya Namtumbo mkoani hapa, ambaye
alikuwa anatumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana
na hatia katika kosa la kuvunja na kuiba mifugo.
Pia aliwataja waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni, Shida
Haulle mzaliwa wilaya ya Mbinga ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kifungo cha
mwaka mmoja jela, baada ya kupatikana na hatia katika kosa la wizi.
Wengine ni Mhamudu Msusa mkazi wa Nandembo wilayani Tunduru
ambaye alikuwa anatumikia kifungo cha mwaka mmoja, sawa na marehemu Mtewa
kwa kosa la kuiba kuku.
Kamanda Mwombeji pia alimtaja majeruhi mwingine, aliyekumbwa
na mkasa huo kuwa ni Akandu Abdallah mkazi wa kijiji cha Mchoteka wilayani
Tunduru ambaye alikuwa anakabiliwa na adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela,
baada ya kupatikana na hatia katika kosa la kujifanya usalama wa Taifa.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya serikali wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma, Dkt. Mmari Zabron alithibitisha kuwapokea marehemu hao wawili na
majeruhi watatu, Marchi 18 mwaka huu majira ya saa 1 usiku.
Alisema baada ya kuwapokea miili ya marehemu hao, ilihifadhiwa
katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo katika hospitali hiyo.
Kuhusiana na hali za majeruhi hao, alisema kuwa juhudi za
kuokoa maisha yao zinaendelea na kwamba hali zao kwa sasa zilikuwa zinaendelea
kuimarika baada ya kupatiwa matibabu.
Mganga aliyeifanyia uchunguzi miili ya marehemu hao, Dkt.
Gaofrid Mvile alisema kuwa vifo hivyo vilisababisshwa na mshituko wa shoti ya
umeme uliosababishwa na radi hiyo.
Taarifa ambazo zilithibitishwa kutoka kwa baadhi ya askari wa
gereza hilo, ambao walizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, kwa madai
kuwa wao sio wasemaji wa Jeshi hilo, zinaonesha kuwa ni tukio la nne kwa radi
kupiga katika gereza hilo.
Walisema mwaka 2014 radi ilipiga mti mkubwa uliokuwa jirani
na gereza lao, mwaka 2015 ilipiga na kuua ng'ombe mmoja na mwaka huu imepiga tena
na kusababisha matatizo hayo yaliyotokea jambo ambalo linawafanya waishi kwa
hofu.
Kufuatia hali hiyo askari hao wameiomba serikali, kuangalia
uwezekano wa kuwafungia vifaa vinavyoweza kusaidia kudhibiti radi hizo, ili
zisiendelee kusababisha maafa katika makambi yao na gereza kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment