Na Steven Augustino,
Tunduru.
WATU wanaodaiwa kuwa ni majambazi, wamemuua kwa kumpiga risasi
Mwenyekiti wa kitongoji cha Chilundundu, Zubery Mohamed (53) na kufanikiwa
kumpora kiasi cha shilingi 80,000.
Sambamba na mauaji hayo, pia majambazi hao walipiga risasi nne
hewani na kufanikiwa kupora kiasi cha shilingi 470,000 mali ya Mkalela Muhidin
(28) tukio ambalo lilifanyika, majira ya usiku.
Zubery Mwombeji. |
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Marchi 11mwaka huu,
katika kitongoji hicho kijiji cha Misechela wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.
Baadhi ya mashuhuda walisema kwamba, katika matukio yote majambazi
hao walitumia bunduki aina ya SMG na kwamba katika tukio la kwanza lililotokea
kwenye kitongoji cha Mkalela kijiji cha Misechela, maharamia hao walifyatua
hewani risasi na kufanya uporaji huo wa shilingi 470,000.
Walisema katika tukio la pili maharamia hao, walimpiga risasi
nne na kumuua Mohamed wakati akiwa anatumia upanga ili kuweza kupambana na majambazi
hao, majira hayo ya usiku.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji
amethibitisha kuwepo kwa matukio hayo na kwamba tayari kuna watu watatu
wanashikiliwa ambao wanadaiwa kuhusika na mauaji hayo, na majina yao
yamehifadhiwa kwa sababu za kiusalama kutokana na uchunguzi bado unaendelea
kuhusiana na matukio hayo.
Alisema katika
kuhakikisha kuwa wanakamilisha kazi hiyo kwa haraka, tayari amekwisha tuma
viongozi waandamizi wa jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina,
ili kubaini ukweli uliopo juu ya matukio hayo.
Alisema ametoa maelekezo kwa jeshi la Polisi wilayani
Tunduru, kuendesha msako mkali ili kuweza kuwanasa watuhumiwa hao na
kujiridhisha juu ya mambo hayo, yanayohatarisha usalama wa watu na mali zao.
Kamanda Mwombeji ametoa wito pia kwa wananchi, wenye taarifa
zitakazofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao kwa lengo la kulisaidia jeshi
hilo, ili liweze kuwakamata kabla ya kuleta madhara kwa watu wengine.
Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Mohamed, Dkt.
Titus Tumbu alisema kuwa chanzo cha kifo hicho kilisababishwa kutokwa na damu
nyingi baada ya risasi hizo kupenya kutoka upande wa bega la kulia, yaani
kifuani na kutokeza upande wa nyuma kati kati ya mgongo wake.
No comments:
Post a Comment