Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani Ruvuma,
imempongeza Rais John Magufuli kwa kazi anazozifanya za utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitendo ambacho kimeelezwa kuwa kufanya
hivyo ni kujenga imani kwa wananchi na serikali yao.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa UWT mkoani humo, Kuruthumu
Mhagama alipokuwa kwenye kikao cha baraza maalumu la jumuiya hiyo
kilichofanyika mjini hapa, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kuruthumu alisema serikali ya awamu ya tano, chini ya kauli
mbiu ya Hapa kazi tu imedhamiria kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi wake na
kwamba kinachotakiwa sasa, kila mwananchi ahakikishe anatekeleza majukumu yake
ipasavyo kwenye eneo lake ili dhamira ya serikali kuwaletea maendeleo iweze
kutimia.
Mhagama alisema kuwa pia uamuzi wa Rais kumchagua makamu wake,
Samia Suluhu Hassan lilikuwa ni jambo jema ambalo limeendelea kuwapa msukumo
mkubwa wanawake, hasa ikizingatiwa kuwa tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961
hajawahi kuchaguliwa mwanamke kuongoza nafasi hiyo.
“Nachukua nafasi hii kwa niaba ya wanachama wote wa UWT
mkoani hapa, kuwapongeza na kuwashukuru wanachama wote wa CCM kwa kumpigia kura
za ndio Rais Magufuli, lakini pia ni muhimu sisi kama wanawake tumshukuru kwa
uamuzi wake wa kumteua makamu wa rais mwanamke”, alisema Kuruthumu.
Kuruthumu alisema kwamba Umoja huo wa wanawake hapa Ruvuma
umedhamiria kuendelea kuhamasisha wanawake, ambao sio wanachama wa jumuiya hiyo
wajiunge sambamba na kutekeleza umuhimu wa kulipa ada zao za uanachama kwa
wakati.
Alisema madiwani wa viti maalumu naom wanapaswa kutekeleza
majukumu yao ya utekelezaji wa ahadi zao, ambazo walizitoa wakati wa kampeni za
uchaguzi mkuu uliopita, ili wananchi waweze kujenga imani nao ikiwemo chama na
serikali kwa ujumla.
Hata hivyo alitahadharisha juu ya wanachama wenye tabia ya
kukisaliti chama wakati wa chaguzi mbalimbali, kitendo ambacho katika uchaguzi mkuu
uliofanyika mwaka jana kulijitokeza katika baadhi ya maeneo, kupoteza kata na
majimbo.
No comments:
Post a Comment