Na Steven Augustino,
Tunduru.
NAIBU Waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi
Edwin Ngonyani, ameamuru kuvunjwa mara moja kituo cha kuuza mafuta cha kampuni
ya Cross roads, ambacho kinamilikiwa na Saleh Ahamad mjini Tunduru mkoani
Ruvuma, ili kupisha ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Aidha Waziri huyo pia amemwagiza Katibu tawala wa wilaya hiyo,
Ghaib Lingo kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
wilayani Tunduru, kufanya uchunguzi juu ya uhalali uliotumika kumpatia kibali
cha kujenga kituo hicho katika eneo ambalo sio rasmi.
Kwa mujibu wa maagizo hayo, Ngonyani ameagiza hatua kali
zichukuliwe kwa wahusika wote ikiwa ni pamoja na kuwataka kumlipa fidia ya
hasara atakayoipata, kutokana na zoezi hilo la uvunjaji litakapofanyika.
“Haiwezekani serikali
ibebe mzigo kutokana na uzembe wa watu wengine, kuruhusu kujenga vituo vya
mafuta katika maeneo ambayo siyo rasmi na barabara inatakiwa ipite", alisema
Ngonyani.
Ngonyani alitoa maagizo hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi
hapa mkoani Ruvuma, iliyoambatana na ukaguzi wa ujenzi wa barabara inayoendelea
kujengwa kwa kiwango cha lami kutoka Songea kwenda Tunduru na Tunduru kuelekea Masasi,
ikiwani ni juhudi ya serikali kutaka kufungua mikoa ya Kusini ipitike kwa
urahisi.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wakandarasi wanaojenga
barabara hiyo, Meneja wa wakala wa barabara (TANROADS) mkoa humo, Mhandisi
Mathew Mtegumle aliwataka wakandarasi hao kuongeza bidii katika ujenzi huo na
kuhakikisha kwamba, barabara hiyo inakamilika kwa wakati.
Naye Katibu tawala wa wilaya ya Tunduru, Ghaib Lingo pamoja
na kuyapokea maelekezo hayo aliahidi kufuatilia, kuyasimamia na
kuhakikisha zoezi hilo linatekelezwa kwa wakati.
No comments:
Post a Comment