Na Steven Augustino,
Tunduru.
MKAZI mmoja wa kijiji cha Mabatini, wilayani Tunduru mkoa wa
Ruvuma Omary Rashid (64) amekutwa akiwa amefariki dunia, katika tukio la kugongwa
na gari au pikipiki.
Zubery Mwombeji. |
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema waliuona mwili wa marehemu huyo
ukiwa umelala barabarani eneo la mabatini jambo ambalo liliwafanya wahisi kwamba,
huenda marehemu aligongwa na vyombo hivyo vya moto.
Mtoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Abdala Issa,
alisema kuwa huenda chanzo cha kifo chake kilisababishwa na tabia yake ya ulevi
wa kupindukia na kwamba, baada ya kuzidiwa na pombe alilala barabarani na hivyo
kugongwa bila kujitambua.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha
kuwepo kwa tukio hilo na wanaendelea kufanya uchunguzi, ili kuweza kujua chanzo
cha kifo chake.
Aidha alisema wamejipangga kufanya uchunguzi wa kina kwa
lengo la kuhakikisha kwamba, mtuhumiwa aliyefanya kosa hilo anakamatwa na sheria
kuchukua mkondo wake.
Kufuatia hali ya utata uliopo juu ya tukio hilo, Kamanda Mwombeji
alisema Polisi wanawaomba wananchi wenye taarifa za tukio hilo kutoa
ushirikiano wa karibu, ili waweze kumkamata mhusika kwa urahisi zaidi.
Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Rashid, Dkt.
Gaufrid Mvile alisema kuwa kifo hicho kilisababishwa na kutokwa na damu nyingi,
baada ya ajali hiyo kutokea.
Dkt. Mvile alifafanua kuwa, marehemu alivunjika mguu wa
kushoto na kuvurugika mbavu za pande zote mwilini mwake, pamoja na kupasuka
fuvu la kichwa chake.
No comments:
Post a Comment