Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho amesema
kwamba uzalishaji wa zao la mpunga katika wilaya hiyo umeongezeka kutoka
tani 50,000 mwaka 2012 sawa na tani 2 kwa hekta, hadi kufikia tani
143,375 kwa mwaka 2015 ambayo ni wastani wa tani 4
kwa hekta moja, jambo ambalo limeifanya wilaya hiyo kukua
kiuchumi na kupunguza umaskini kwa wananchi wake.
Zao la Mpunga. |
Ongezeko hilo la uzalishaji alifafanua kuwa limetokana
na zao hilo kuwa la kibiashara zaidi, hasa baada ya kupatikana kwa soko
kubwa mikoa jirani ya Lindi na Mtwara ambako mahitaji ya mchele ni
makubwa ikilinganishwa na matumizi yaliyopo ndani ya wilaya hiyo, hivyo
kuwepo kwa wafanyabiashara wengi wanaokwenda kununua na kufanya thamani ya zao
hilo kukua.
Nalicho alisema hayo alipokuwa akizungumza na
gazeti hili ofisini kwake, kuhusiana na hali ya chakula na
shughuli za maendeleo, katika sekta ya kilimo zinavyoendelea wilayani humo.
Aidha alieleza kuwa, kuongezeka kwa skimu ya
kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya mbolea na zana bora za kilimo chini
ya mpango madhubuti wa kuongeza uzalishaji wa chakula na mazao ya
biashara, unaofanywa na halmashauri ya wilaya hiyo ndiyo umeleta ufanisi mkubwa
katika uzalishaji wa zao la mpunga na kuifanya wilaya ya Namtumbo, kujitosheleza
kwa chakula ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2014/2015 hekta 251,431.3
kati ya hekta 263.369 ndizo zilizopangwa kulimwa, ambazo zingeweza kuzalisha
tani 450,631.4 kati ya malengo ya kuzalisha tani 500,174.4 ambazo
walishindwa kuzifikia kutokana na uwepo wa changamoto mbalimbali.
Changamoto hizo alizitaja kuwa ni huduma duni za
usambazaji wa pembejeo, miundombinu hafifu ya umwagiliaji na
pembejeo hizo kuuzwa kwa bei ghali, ambayo wakulima wengi walishindwa kumudu
gharama husika.
No comments:
Post a Comment