Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WANAFUNZI 10 kati ya 106 wanaosoma kidato cha sita, shule ya
sekondari Namabengo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wamesimamishwa kuendelea
na masomo katika shule hiyo kwa muda wa wiki tatu, kutokana na kukosa nidhamu
na kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Maandamano hayo walifanya wakielekea kwa Mkuu wa mkoa huo, Said
Mwambungu kwa lengo la kupeleka malalamiko yao dhidi ya Makamu mkuu wa shule
hiyo, Shaibu Champunga wakimtuhumu kuwa na lugha na tabia chafu na vitisho kwa
wanafunzi hao.
Katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo, Alkwin Ndimbo alipozungumza
na mwandishi wetu alisema kwamba baada ya wanafunzi hao kufanya maandamano
hayo, zilifanyika jitihada za kuwarudisha shuleni kwa lengo la kubaini chanzo
cha maandamano hayo huku akimwagiza Ofisa elimu wa sekondari wilayani humo, Patrick
Atanas ahakikishe anachukua hatua za haraka kwa kukutana na viongozi wa shule
na wanafunzi hao, ili kuona tuhuma zinazomkabili Makamu mkuu wa shule hiyo.
Ndimbo alieleza kuwa, baada ya Ofisa elimu Atanas na uongozi
wa shule na wanafunzi wote kukaa pamoja na kuangalia chanzo cha tatizo hilo ilibainika
kuwa wanafunzi 106 kutoka Namabengo hadi kijiji cha Mlete, umbali wa kilometa
16 walifanya kosa la kuandamana bila kufuata taratibu husika.
Walisema kitendo hicho ni utovu wa nidhamu na wamevunja
kanuni na sheria za shule hiyo kwa kuondoka eneo la shule bila idhini husika, ambapo
kwa kufanya kosa hilo wanafunzi hao walikiri na uongozi wa shule uliamuru
wanafunzi 96 wachapwe viboko vitatu kila mmoja, huku 10 ambao ndio walikuwa
vinara wa maandamano hayo wamesimamishwa masomo kwa muda wa wiki tatu na mara
watakapomaliza adhabu hiyo watatakiwa waende na wazazi wao, kwa hatua zaidi za
kinidhamu.
Alisema kuwa tuhuma ambazo wanafunzi hao walimtuhumu mwalimu
Champunga, sio za kweli kwani katika mahojiano mbalimbali yaliyofanyika hakuna
aliyeweza kuthibitisha tuhuma hizo, hivyo hawawezi kumchukulia hatua bila kuwa
na ushahidi wa kutosha.
Malalamiko ya watoto hao yalifuatia ikidaiwa kwamba, Champunga
amekuwa akiwatolea vitisho na lugha za matusi kwa wanafunzi, kuwachapa viboko
visivyo na idadi, amekuwa akiingia kwenye bweni la wanafunzi wa kike nyakati za
usiku bila kufuata taratibu na kulazimisha kufanya nao mapenzi akimtoa nje ya
bweni mwanafunzi wa kike anayemtaka.
Kutokana na malalamiko hayo walitaka kwenda kumwona Mkuu wa
mkoa wa Ruvuma, Mwambungu ili aweze kuwasikiliza na kupatia ufumbuzi wa kero
zao na kwamba juhudi za kutaka kuonana na Mkuu huyo wa mkoa, ziligonga mwamba baada
ya kuzuiwa na askari Polisi wa wilaya ya Namtumbo.
Wanafunzi hao walizuiwa wakiwa kijiji cha
Mlete, wakielekea kwa Mkuu huyo wa mkoa ambapo kijiji hicho kipo nje
kidogo ya Manispaa ya Songea ambapo askari Polisi walipoingilia kati, waliamuru
wasimame na kuwataka waeleze sababu ya kufanya maandamano bila kibali, ambapo wanafunzi
hao walieleza kuwa kila mtu ana haki ya kuongea kwa kuwa walishatoa malalamiko
yao kwa Mkuu wao wa shule lakini hawajasikilizwa, hivyo waliona ni vyema
malalamiko yao wakayafikishe kwa Mkuu wa mkoa huo.
Muda mfupi baada ya kuwasili Katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo,
Alkwin Ndimbo na kusikiliza malalamiko ya wanafunzi hao dhidi ya Makamu mkuu wa shule ya sekondari Namabengo, Shaibu
Champunga kwamba hawamtaki shuleni hapo kwa sababu ya vitendo hivyo vichafu
anavyowafanyia.
Pamoja na mambo mengine, walilalamikia pia shule hiyo haina
miundombinu mizuri ambapo walidai kuwa vyoo vilivyopo ni vibovu havifai
kutumika, baadhi ya madarasa hayana sakafu na kwamba wanalazimika kwenda umbali
mrefu kufuata huduma ya maji.
Baada ya viongozi hao kusikiliza malalamiko ya wanafunzi hao,
waliwataka warudi shuleni ili wakatoe maamuzi mbele ya wanafunzi wote pamoja na
walimu wao jambo ambalo, wanafunzi walilikubali na kusitisha maandamano hayo.
No comments:
Post a Comment