Na Muhidin Amri,
Songea.
KUELEKEA siku ya wananawake duniani ambayo kila mwaka inafanyika
Marchi 8, serikali imeombwa kuongeza nafasi za upendeleo kwa wanawake ili
kuwaongezea uwezo wa kiutendaji, hasa pale wanapoteuliwa kushika
nafasi mbalimbali za uongozi na kuwaongezea nguvu katika kukabiliana na
changamoto zinazowakabili mbele yao katika maisha yao ya kila siku.
Rai hiyo ilitolewa jana mjini Songea na Mwanaharakati wa masuala
ya wanawake na mfanyabiashara maarufu, anayeuza mafuta ya kuendeshea mitambo
mbalimbali mkoani Ruvuma, Farida Mdaula wakati alipokuwa akizungumza
na baadhi ya wanawake wa Manispaa ya Songea, ambao waliamua kushiriki katika
zoezi la usafi wa kuosha magari kwa ajili ya kutafuta fedha za kusaidia
watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wale waliokacha kwenda shule
kwa kukosa mahitaji muhimu.
Alisema wanawake wengi wanakabiliwa na umaskini, hasa wa
kipato na kukosa fursa ya kushirikishwa kwenye vyombo vya maamuzi na hata
katika umilikaji wa rasilimali, licha ya ukweli kwamba ndiyo kundi kubwa linalochangia
maendeleo na kukua kwa uchumi wa nchi yetu.
Kwa mujibu wa Mdaula alisema kwamba, wanawake wakipewa nafasi
katika vyombo hivyo kama vile Makahama, Bunge au nafasi za kuteuliwa ikiwemo
ukuu wa wilaya, mkoa na hata kuwa wakurugenzi wa halmashauri itasaidia kuwa na
uwezo katika kukabiliana na hali ya umaskini kwa kuwa, wale
watakaopata nafasi hizo watajitokeza kuwapa elimu na maarifa
wanawake wenzao.
“Sikatai kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, wakati wa
utawala wa Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete wanawake wamepata
nafasi nyingi za uongozi katika nchi hii, hata hivyo sisi kama wanawake
tunahitaji nafasi hizo ziongezwe zaidi ili tuweze kuwa sawa na wanaume”, alisema
Mdaula.
Vilevile aliwataka wanawake kuushinda moyo wao, kwa
kujiepusha kufanya vitendo ambavyo vinawavunjia heshima mbele ya jamii badala
yake wafanye kazi halali za kujipatia kipato, ikiwemo kazi ya
kuosha magari ambayo kwa sasa ina faida kubwa kutokana na
kuongezeka kwa idadi kubwa ya magari.
Mbali na hilo, Mdaula amewashauri wanawake wa mkoa huo na
kote nchini kujitokeza kukopa fedha katika taasisi za fedha kama vile mabenki, vyama
vya kuweka na kukopa ili waweze kuanzisha miradi ya kiuchumi, itakayoweza
kuwafanya waendeshe maisha yao na sio muda mwingi kuishi kwa kuwategemea waume
zao.
“Wanawake ni muhimu sana, waache tabia ya kizamani ya
utegemezi kwa wanaume, kwani licha ya kuwa mume ndiyo mwenye wajibu wa kutafuta
riziki ya kila siku kwa ajili ya familia, hata hivyo na sisi tusikae na
kusuburi kutoka kwao kwani tutaendelea kukabiliwa na umaskini
katika maisha yetu”, alisema.
Katika hatua nyingine Mdaula, amewaonya wanawake kuacha tabia
ya kupigana majungu na hali ya kukatishana tamaa wakati huu ambao bado
kundi hilo linakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, ikilinganishwa na wanaume
hivyo ni muhimu wapeane moyo na kufarijiana hasa pale mmoja wao anapopata
matatizo.
Pamoja na mambo mengine, Mdaula ambaye pia ni kada maarufu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa mkoani Ruvuma, amewakumbusha wanawake wenzake kuwa
mstari wa mbele kupeleka watoto wao shule badala ya kuwafanyisha kazi za
nyumbani, ambazo kwa muda mrefu zimekwamisha ndoto za vijana wengi kuendelea
na maisha yao katika kupiga mbele hatua mbalimbali.
No comments:
Post a Comment