Menas Mbunda Andoya enzi ya uhai wake, akiwa na mkewe na Waziri Mkuu Mizengo Pinda
wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuzalisha umeme vijijini, ambao ulibuniwa miaka
13 iliyopita.
|
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SHIRIKA la ugavi nishati ya umeme Tanzania (TANESCO) limeagizwa
kujenga ushirikiano na kampuni binafsi ya Andoya Hydro Electric Power (AHEPO)
ambayo inazalisha umeme utokanao na nguvu ya maji wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, ili mradi huo uweze kuwa endelevu.
Aidha umeme huo wa maporomoko ya maji umeunganishwa katika
njia kuu ya gridi ya TANESCO ambao husambazwa kwa wateja waliopo wilayani humo.
Waziri wa nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa
agizo hilo juzi alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mkurugenzi
wa kampuni ya AHEPO, Alex Andoya alimweleza Waziri Muhongo kuwa madhumuni ya
kuzalisha umeme katika mradi huo ni Megawati 1 na umeunganishwa kwa wateja wa
awali 922 kati ya 3,835 katika vijiji vya Lifakara, Kilimani na Mbangamao
wilayani Mbinga na ziada huuzwa katika shirika hilo la ugavi wa umeme ukilenga
kupata umeme kwa njia endelevu na bei nafuu.
“Hivi sasa tayari ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme
kutoka Mbinga mjini, hadi kituo kikuu cha uzalishaji na usambazaji katika vijiji
hivyo umekwisha kamilika”, alisema Andoya.
Alifafanua kuwa mwaka 2005 kampuni hiyo ya Andoya Hydro
Electric Power ilisajiliwa na upembuzi yakinifu wa mradi ulikamilika, hatimaye
taarifa na mchanganuo wa mradi ulipitiwa na wataalamu mbalimbali wa taasisi za
serikali ikiwamo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania TANESCO, NEMC, EWURA na wataalamu kutoka benki ya dunia nao wote waliafiki
kuwa kiasi cha Megawati 1 kinaweza kupatikana katika maporomoko hayo yaliyopo
katika mto Mtandasi.
Kufikia Novemba 2012 mradi ulifanikiwa kupata kibali na fedha
za kutekeleza, ukiwa katika hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa njia ya
usafirishaji wa umeme yenye urefu wa kilometa 14 kwa kiwango cha HT kutoka
kituo cha umeme cha Mbangamao hadi makao makuu ya wilaya ya Mbinga, na sasa
umeunganishwa na gridi ya TANESCO wilayani humo, pamoja na vijiji vya Lifakara,
Kilimani na Mbangamao.
Andoya alieleza kuwa awamu ya pili ilikuwa ni ujenzi wa njia
za kusambaza nishati hiyo muhimu kwa wateja, ambapo gharama za ujenzi wa mradi
huo umegharimu shilingi bilioni 4.5 na kwamba asilimia 30 zilichangwa kutoka
mtaji wa kampuni hiyo ya AHEPO, asilimia 70 ni mkopo kutoka benki ya CRDB na mkopo
wa benki ya dunia kupitia serikali na taasisi zake ikiwamo (REA) chini ya
mpango wa Tanzania Energy Development and Access Project (TEDAP) ambapo pia
UNIDO nao walichangia dola 250,000 za Marekani.
No comments:
Post a Comment