Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim
Majaliwa amemuagiza Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu ahakikishe kwamba kabla
hajamaliza ziara yake ya siku tatu anahitaji kuonana na viongozi wa Chama Kikuu
cha Ushirika cha Tumbaku wilaya ya Songea na Namtumbo (SONAMCU) mkoani humo.
Agizo la Waziri mkuu huyo, amelitoa leo wakati alipokuwa
Ikulu ndogo ya Songea kufuatia kusuasua kwa uzalishaji wa zao la tumbaku na
kutofanya kazi kwa muda wa miaka 18 kiwanda cha kusindika zao hilo kilichopo
Manispaa ya Songea mkoani hapa.
“Kabla sijamaliza ziara yangu, nahitaji kuonana na viongozi
wote wa chama hiki kikuu cha uzalishaji wa tumbaku na mwakilishi mmoja mmoja
kwa kila mkulima, ili niweze kupata mpango wao mkakati wa uendelezaji wa zao
hili sambamba na ufufuaji wa kiwanda”, alisisitiza Majaliwa.
Kiwanda cha kusindika tumbaku ambacho kinajulikana kwa jina
la SONTOP kilichopo katika Manispaa hiyo, kilisimama kusindika zao hilo
kufuatia kuingiwa kwa mikataba mibovu kwa baadhi ya viongozi iliyoambatana na
ubadhirifu wa fedha ambao ulisababisha kiwanda hicho kishindwe kujiendesha.
Aidha katika mikataba hiyo, ambayo ina makampuni yanayonunua
zao hilo mkoani Ruvuma, iliweka masharti ya kusindika tumbaku kwa kutumia
viwanda vilivyoko mkoani Morogoro jambo ambalo mkoa huo hauzalishi zao hilo na
kwamba umesababisha kupoteza ajira za vijana takribani 2,500 waliokuwa
wakifanya kazi katika kiwanda hicho.
Waziri Mkuu Majaliwa ameshangazwa pia na uongozi wa chama
hicho kikuu cha ushirika cha SONAMCU, kutaka kulitumia eneo la kiwanda hicho
cha kusindika tumbaku kilichopo mjini Songea, kujenga vibanda vya biashara
badala ya kufikiria ni namna gani watafufua kiwanda hicho.
Vilevile Majaliwa alishitushwa na hali hiyo ambayo
imesababisha kushuka kwa uzalishaji wa zao la tumbaku mkoani humo, ambalo
lilikuwa ni tegemeo kubwa kwa kukuza uchumi wa wananchi wa wilaya za Namtumbo,
Songea na Mbinga.
Kadhalika wakati haya yote yakitokea, mkoa wa Ruvuma
unategemea sekta ya kilimo ambapo wakazi wake asilimia 90 ni wakulima, huku
dhamira ya serikali ya awamu ya tano ikionesha kusimamia kikamilifu sekta ya
kilimo chenye tija nchini sanjari na ufufuaji wa viwanda ili kuifikisha nchi
katika uchumi wa kati.
Hata hivyo kuwepo kwa sakata hilo, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma
Said Mwambungu alimweleza Waziri Mkuu kwamba, tayari hatua za kisheria
zimechukuliwa dhidi ya viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika na chama kikuu
SONAMCU wanaodaiwa kuhusika na ufisadi huo, tayari wamefikishwa Mahakamani.
No comments:
Post a Comment