Na Kassian Nyandindi,
Songea.
SERIKALI hapa nchini imesema kuwa, itaweka mpango mzuri wa
kuhakikisha kwamba kila mwananchi katika maeneo anayozalisha kilimo cha mazao
ya chakula na biashara, anahamasishwa alime mazao yake shambani kwa kutumia matrekta
na kuachana na jembe la mkono ili mazao hayo waweze kuzalisha kwa wingi.
Aidha imeelezwa kuwa mpango huo unaweza kuwafikia wakulima
hao kwa urahisi, endapo viongozi waliopo madarakani katika ngazi za halmashauri
ya wilaya hadi mkoa, wataweza kuweka mikakati madhubuti katika bajeti zao kwa
kuhakikisha kwamba wakulima wanapewa matrekta hayo ya kulimia kwa gharama
nafuu.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa
Kassim Majaliwa alisema hayo hivi karibuni mjini Songea akiwa katika ziara yake ya siku
tatu mkoani humo, akiwajibika kupita katika maeneo mbalimbali kuona hali
halisi ya maendeleo na kuweka msisitizo wa namna ya utendaji kazi.
“Tutatumia mkoa wenu wa Ruvuma kama mfano ndani ya nchi, kupitia
kilimo mmeweza kuwa watano kitaifa katika kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja,
hivyo basi nasisitiza maeneo yote ya mabondeni, tuwahamasishe pia wananchi
waendeshe kilimo cha umwagiliaji, kuna kila sababu kwenye eneo hili tuhakikishe
tunajikita zaidi”, alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Pia alieleza kuwa kutokana na wananchi wa mkoa huo kuonekana
wengi wao wana kipato kizuri, hivyo wanapaswa kuwa na matumizi mazuri ya fedha
ili waweze kujiletea maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Licha ya kujishughulisha na kilimo, pia ameuagiza uongozi wa
mkoa huo kupitia viongozi husika wa halmashauri uelekeze wananchi katika suala
la ufugaji nyuki ili nalo liweze kuwaingizia mapato makubwa.
Waziri Mkuu huyo amewaagiza pia Wakurugenzi wa Halmashauri
hapa nchini, kupima mashamba ya wakulima wa kawaida ili waweze kupata hati
miliki na hatimaye mwananchi aweze kukopesheka na taasisi za kifedha kwa lengo
la kusukuma maendeleo yake mbele.
“Naagiza mkae kwenye halmashauri zenu na kutekeleza jambo
hili haraka, tuache tabia ya kuazima wapimaji ardhi kutoka maeneo mengine vifaa
vya kupimia iwe agenda muhimu katika bajeti zenu ni wajibu kuwa navyo, ili
viweze kuturahisishia utekelezaji wa jambo hili”, alisema.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa
mkoa huo Said Mwambungu alisema kuwa mkoa wake kwa mwaka unazalisha tani 689,123
za mazao ya chakula na hilo linatokana na kuimarika kwa matumizi ya pembejeo,
zana za kilimo na matumizi bora ya ugani.
Sekta ya elimu:
Kadhalika Waziri Mkuu Majaliwa, alipozungumzia juu ya sekta
ya elimu Wakuu wilaya mkoani humo amewataka kuchukua hatua madhubuti, juu ya kumaliza
tatizo la uhaba wa madawati ya kukalia wanafunzi darasani kwa kutumia
rasilimali za misitu waliyonayo katika maeneo yao, ili kuwaondolea adha watoto
hao ya kukaa chini.
Alisema lazima wafanye uhakiki wa matengenezo ya madawati hayo
kwa shule zote za msingi na sekondari, ili tatizo hilo katika kipindi cha mwaka
huu liweze kwisha na serikali haitarajii kusikia tena mkoa huo, unakuwa na mapungufu
ya madawati ya kukalia watoto shuleni.
Alisema kuwa wakuu wa wilaya, wakae na Wakurugenzi wao katika
halmashauri kupitia vikao husika na kuona namna gani wanatumia sheria za
uvunaji misitu iliyopo katika maeneo yao, ili waweze kupata mbao za kutengenezea
madawati hayo.
Vilevile alisisitiza kwamba kila mtoto mwenye umri wa miaka
minne hadi mitano, wahakikishe wanaandikishwa na kupelekwa shule kwa ajili ya
kuanza chekechea na kila ilipo shule ya msingi, wahakikishe panakuwa na darasa
la chekechea ili kuweza kumsaidia mwananchi wa kawaida aweze kupeleka mtoto
wake shule.
Aliongeza kuwa zoezi hilo liendane sambamba na ujenzi wa
nyumba za walimu na huku akisisitiza shule za msingi hadi sekondari, serikali
imefuta ada na baadhi ya mlundikano wa michango ambapo fedha zote za kuendeshea
shule hizo, serikali itapeleka moja kwa moja katika shule husika na tayari
akaunti za shule zote hapa nchini, zimekwisha chukuliwa kwa ajili ya
utekelezaji wa zoezi hilo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma:
Said Mwambungu ambaye ni Mkuu wa mkoa huo, awali akisoma taarifa
ya maendeleo ya mkoa katika sekta ya elimu alisema kuwa kutokana na watoto
wengi kuandikishwa kujiunga na darasa la kwanza, kuna upungufu mkubwa wa
madawati ambapo mahitaji ni 120,812 yaliyopo ni 76,025 na kufanya upungufu wake
kuwa ni 44,787.
Mwambungu alifafanua kwamba kumekuwa pia na upungufu wa
nyumba za walimu, ambapo mkoa unahitaji nyumba za walimu wa shule za msingi
7,499 na sekondari 2,655 na zilizopo kwa shule za msingi kwa sasa ni 2,574
upungufu wake ni 4,925 kwa sekondari zilizopo sasa ni 515 pungufu yake ni
2,140.
Alieleza kuwa katika kutatua tatizo hilo, mkoa umejipanga
kuhamasisha wananchi na halmashauri zake kuwa na benki ya tofari 100,000 kwa
ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba hizo.
Tatizo la mimba lipo katika shule za sekondari ambapo kwa
mwaka 2014, wanafunzi 56 walishindwa kuendelea na masomo yao kutokana na kupata
ujauzito, na kwa upande wa shule za msingi wanafunzi 9 walikuwa na hali hiyo
katika kipindi cha mwaka jana na wote, hawakuweza kufanya mitihani yao ya
mwisho kutokana na kukumbwa na hali hiyo.
No comments:
Post a Comment