Na Kassian
Nyandindi,
Ruvuma.
MADAKTARI na Wahudumu wa afya wanaofanya kazi katika
Hospitali ya Rufaa mkoani Ruvuma, wamejikuta wakiwa katika wakati mgumu baada
ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, kuwajia juu na
kukemea vitendo vya utoaji mimba ambavyo vimeshamiri katika hospitali hiyo.
Hali hiyo ilijitokeza katika ukumbi wa mikutano wa hospitali
hiyo, ambapo Waziri Mkuu Majaliwa alimweleza Mganga mkuu, Daniel Malekela
kwamba watumishi wake hasa madaktari wamekuwa na mazoea ya kufanya vitendo hivyo
hasa kwa wanafunzi wanaosoma shule ya msingi na sekondari.
“Mganga Mkuu, hospitali yako inayosifa ya kutoa mimba,
madaktari wamekuwa wakitumia wodi namba tano kufanyia kazi hii sasa natoa onyo
kali ni marufuku kuanzia leo, sitaki kusikia tena jambo hili nitawafukuza kazi
na kuwafunga”, alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu huyo alifafanua kuwa utoaji mimba, umekuwa ukifanyika
hata katika jengo la upasuaji lililopo hospitalini hapo na kuongeza kuwa jambo
hilo hataki kuliona linarudia tena na kwamba, hatakuwa na msamaha wowote kwa
atakayehusika na kitendo hicho.
“Nyiee………… ole wenu, Mganga mkuu na Mganga mfawidhi wa
hospitali ya mkoa wa Ruvuma, hakikisheni hili jambo halijitokezi tena,
likiendelea nitaanza kuwawajibisha ninyi”, alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu huyo wakati alipokuwa ametembelea wodi za
hospitali ya Rufaa ya mkoa huo, alijionea changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu
wa majengo na malalamiko mbalimbali yaliyojitokeza kutoka kwa akina mama ambao
walikuwa wakiuguza wagonjwa wao.
Akina mama hao kwa nyakati tofauti walimweleza kuwa wamekuwa
wakikaripiwa na kutolewa lugha chafu, kutoka kwa baadhi ya waganga na madaktari
wanaowahudumia jambo ambalo limekuwa kero kwao.
“Mmoja wa wagonjwa alimweleza Waziri Mkuu Majaliwa kwamba, “mimi
binafsi hapa ninamgonjwa wangu amelazwa lakini naambiwa hakuna dawa nakwenda
duka la dawa muhimu kununua ili mgonjwa wangu atibiwe, licha ya kununua dawa husika
mganga wa zamu bado anataka nimpatie fedha ili ahudumie mgonjwa wangu je, hapo
kuna haki”?, alihoji Rosemary Ngonyani.
Vilevile katika wodi ya watoto, walilalamikia kitendo cha
watoto wao ambao ni wagonjwa kulazwa wawili wawili katika kitanda kimoja na
kuiomba serikali iangalie kwa jicho la huruma tatizo hilo, ili liweze kupatiwa
ufumbuzi.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Majaliwa alimuagiza Katibu tawala
wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko ahakikishe kuwa mkoa wake unatenga bajeti
kwa ajili ya kupata fedha za kukarabati majengo ya hospitali hiyo ya rufaa na
ujenzi wa majengo mengine mapya, ili kuweza kukidhi haja na kuondoka na kero ya
kulala kitanda kimoja wagonjwa wawili.
Hata hivyo alitoa onyo kwa wanaotoa vifaa vya matibabu vya
serikali na kuvipeleka kwenye zahanati, vituo vya afya au hospitali binafsi
huku akijua kwamba ni kinyume na utaratibu atakayebainika atachukuliwa hatua
ikiwemo kufukuzwa kazi.
No comments:
Post a Comment