Na Steven Augustino,
Tunduru.
JUMLA ya shilingi milioni 129,125,000 zimepokelewa wilayani
Tunduru, mkoa wa Ruvuma ili zeweze kutumika katika shughuli za utoaji wa elimu
bure kulingana na ahadi iliyotolewa na Rais wa awamu ya tano, Dkt. John Pombe
Magufuli.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Agnes Hokororo
wakati alipokuwa akizungumza hivi karibuni na wataalamu wake katika kikao cha
kazi kilichofanyika ukumbi wa Klasta ya walimu wa tarafa ya Mlingoti mjini hapa.
Aidha Hokororo aliwatahadharisha watendaji hao kwamba
fedha hizo ni za moto, unaowaka na kiongozi atakayejidai kuchakachua ajiandae
kuunguzwa na moto huo.
Katika kikao hicho Mkuu huyo wa wilaya alikuwa akizungumza na
wakuu wa idara za halmashauri ya wilaya hiyo, wakuu wa shule za sekondari 21 na
msingi, waratibu elimu kata ambao pia alikuwa anawapa maelekezo hayo juu ya matumizi
ya fedha hizo.
Alisema kwa mwaka huu, wilaya yake tangu ianzishwe mwaka 1905 imepokea fedha nyingi tofauti na miaka iliyopita.
Hokororo alitumia nafasi hiyo kwa kuwataka watumishi wake, kusimamia
ipasavyo maelekezo wanayopewa na serikali ili kuweza kufikia malengo
yaliyokusudiwa.
Katika maelekezo hayo pia aliwataka watumishi hao kwenda
kutoa maelekezo ya kina kwa wazazi na walezi wa watoto hao, ili kuwaondolea dhana
potofu ambayo inaonekana kujengwa kuwa elimu bure itaweza kuwanunulia hadi sare
za watoto hao jambo ambalo sio la kweli.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru,
Tina Sekambo aliwasihi watumsihi hao kufanya kazi za utumishi wa umma kwa uwazi
ikiwa ni pamoja na kubandika taarifa za mgawanyo na matumizi ya fedha zote, zinazopokelewa
katika shule zao.
No comments:
Post a Comment