Na Bashir Yakub,
TUNAPOZUNGUMZIA mgogoro wa ardhi tunazungumzia
mgogoro katika viwanja, mashamba, nyumba na majengo.
Wengi wetu tunapokutwa na migogoro ya
ardhi hukimbilia Mahakama za wilaya au
Mahakama kuu ya ardhi, lakini tunasahau
kuwa lipo baraza la ardhi la kata
ambalo baadhi ya migogoro haifai kwenda
huko wilayani au mahakama kuu kabla ya
kupitia hatua hiyo. Sasa makala haya yataelezea
kuhusu baraza la ardhi la kata na
mashauri yanayotakiwa kuanzia hapo.
1. NGUVU YAKE NI KATIKA KATA
TU.
Baraza la ardhi la kata ni
mahakama ya ardhi katika kata husika. Hii
ni kwa mujibu wa kifungu cha 10 ( 1 )
cha sheria ya mahakama za usuluhishi wa
migogoro ya ardhi.
Baraza hili mipaka yake ni
katika kata husika kwa maana kwamba mipaka
ya kata ndio mamlaka yake kijiografia, kila
kata hutakiwa kuwa na baraza lake la
usuluhishi wa migogoro ya ardhi na baraza la
ardhi la kata fulani haliwezi kuvuka
mipaka na kwenda kuamua mgogoro wa
ardhi wa kata nyingine.
2. JE INATAKIWA WAAMUZI WANGAPI
KATIKA BARAZA.
Unapokuwa na mgogoro katika baraza
hili ni muhimu kujua ni watu wangapi
wanatakiwa kuamua mgogoro wako. Mara
kadhaa hasa huko vijijini waamuzi katika
mabaraza haya wamekuwa wakijikalia tu na
kutoa maamuzi pasipo kuzingatia akidi.
Unapaswa kujua kuwa kuna akidi
maalumu ya kisheria na hivyo kabla ya
kuamuliwa mgogoro wako ni vyema
ukahoji akidi hasa ikiwa haijatimia.
Kifungu cha 14( 1 ) kinasema kuwa vikao
vya usuluhishi vya baraza vitakaliwa
na wajumbe wasiopungua watatu huku
mmoja akitakiwa kuwa mwanamke. Hii ni
akidi ya kisheria na hivyo yafaa ujue
kuwa unayo haki ya kuhoji ikiwa akidi
hii haijatimia.
Ni muhimu kutoruhusu kikao
kuendelea ikiwa akidi haijatimia kwa kuwa
maamuzi yatakayotolewa na akidi pungufu kisheria
yatakuwa batili. Kwa hiyo hata kama umeshinda
ushindi wako utakuwa ni kazi bure.
3. JUMLA YA WAJUMBE.
Kifungu cha 11 cha sheria
ya mahakama za usuluhishi wa migogoro
ya ardhi kinasema kuwa baraza la
usuluhishi litakuwa na wajumbe wasiopungua wa nne
na wasiozidi nane. Kati yao watatu
inabidi wawe wanawake, hawa ni wajumbe wa
jumla ambao ndio huunda baraza zima. Zingatia hili
sio akidi ya kila kikao, ila ni wajumbe
kwa ujumla wao.
4. KAZI KUU YA BARAZA.
Kazi kubwa ya baraza la
ardhi la kata imeelezwa vyema katika
kifungu cha 13 ( 1 ) cha sheria ya mahakama
za usuluhishi wa migogoro ya ardhi.
Kifungu kinasema kuwa kazi ya msingi
ya baraza ni kutafuta amani na
utulivu katika eneo husika kupitia
kusuluhisha na kuwasaidia wahusika walio katika
migogoro kufikia suluhu, yenye maelewano
katika masuala yanayohusu ardhi.
5. KUZINGATIA MILA WAKATI WA
USULUHISHI.
Kwakuwa baraza hili linahusu
kata sheria imetoa mwanya kwa wasuluhishi
kuhusisha taratibu za kimila katika
kutafuta suluhu. Hii ni kwa kuwa masuala
ya ardhi na usuluhishi kwa kiasi
kikubwa yameambatana na mila. Sheria inaamini kwamba
wasuluhishi watakuwa wanatoka kata husika
basi pia watakuwa wanajua taratibu za
kimila za eneo husika.
Hii ni kutokana na kifungu cha
13 ( 3 ) kinachosema kuwa baraza katika
kufanya kazi zake za usuluhishi litahusisha
kanuni yoyote ya kimila inayohusu
usuluhishi.
Kifungu kinasema kuwa ikiwa taratibu
za kimila hazitatumika, basi kanuni za
maamuzi ya asili ( Principle of natural justice)
zaweza kutumika.
6. BARAZA HALISULUHISHI MGOGORO
UNAOZIDI MILIONI TATU.
Kifungu cha 15 cha sheria
ya mahakama za usuluhishi wa migogoro
ya ardhi kinasema kuwa baraza la kata
halitakuwa na uwezo wa kusuluhisha
mgogoro ambao thamani yake ni zaidi
ya milioni tatu.
Thamani ya mgogoro huangaliwa kwa
kutizama thamani ya ardhi inayogombaniwa, hivyo ardhi
inayogombaniwa ikizidi milioni tatu basi mgogoro
huo hauwezi kuanzia baraza la ardhi
la kata.
MWANDISHI
WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA
NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA SERIKALI LA HABARI LEO
KILA JUMANNE, GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE. ANAPATIKANA
KWA SIMU NAMBA
0784482959,
0714047241
bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment