Na Mwandishi wetu,
Songea.
SERIKALI imesema kuwa, itazichukulia hatua kali baadhi ya
hospitali na vituo vya afya vya serikali ambavyo huwatoza fedha akina mama
wajawazito, watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka mitano na wazee ambao
wanapaswa kupatiwa matibabu bure.
Kauli hiyo imetolewa jana wilayani Songea na Waziri wa afya, maendeleo
ya jamii, wazee na watoto Ummy Mwalimu wakati alipokuwa akizungumza na
watumishi wa hospitali ya rufaa ya Mtakatifu Joseph Peramiho wilayani
humo.
Alisema sera ya afya, huduma za kujifungua, matibabu kwa
wazee na watoto zinatolewa bure hivyo hospitali hazipaswi kuwatoza fedha
makundi hayo badala yake zifuate maelekezo ya serikali, kwani ni utekelezaji
wa ahadi yake wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
Mwalimu alilazimika kutoa ufafanuzi huo, kufuatia taarifa ya
uongozi wa hospitali hiyo kuwa wanawake wanaofika kwa ajili ya huduma za
kujifungua wanalazimika kulipa kiasi cha shilingi 15,000 jambo ambalo ni
kinyume na sera ya afya na maagizo ya serikali.
Aidha ameutaka uongozi wa hospitali hiyo, kuiga mfano mzuri
wa hospitali ya rufaa Songea ambayo inatoa huduma hizo bila malipo, kwani ina
wajibu wa kutoa huduma hizo bila malipo kwa sababu baadhi ya gharama zake kama
vile madaktari wanaolipwa na serikali na dawa zinachangiwa na serikali.
Vilevile amefurahishwa na hatua ya hospitali hiyo, kutumia
baadhi ya malighafi kama vile chupa kwa ajili ya dawa za maji (drip)
zinazotengenezwa hapa nchini badala ya kuagiza nje ya nchi, na hivyo kupunguza
gharama kubwa.
“Nimefurahishwa na hatua ya kutengeneza dawa za maji maji
ninyi wenyewe, nitakwenda kukaa na wataalamu wangu ili na sisi
tuanze kutengeneza wenyewe badala ya kuendelea kuagiza kutoka nje ya nchi”, alisema.
Awali mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Venance Mushi
alisema kuwa licha ya hospitali hiyo kuhakikisha inaendelea kutoa huduma bora
za matibabu kwa bei nafuu, lakini bado wanakabiliwa na changamoto nyingi.
Dkt. Mushi alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uhaba
wa madawa, pamoja na vifaa tiba kutoka kwa makampuni yanayotengeneza vifaa
hivyo, jambo linalosababisha kuingia gharama kubwa kuagiza vifaa kutoka
kwa makampuni mengine yanayojihusisha na uuzaji wa madawa.
Vilevile alisema kuwa, gharama za uendeshaji katika hosptali
ya Peramiho inategemea wafadhili kutoka nje ya nchi na wanachama wachache
wanaochangia huduma za matibabu kwa hiyo ni vema serikali ikaendelea na
utaratibu wa kuiangalia kwa jicho la huruma ili iweze kukabiliana na idadi
kubwa ya wananchi wanaokwenda kupata matibabu.
Kwa mujibu wa Dkt. Mushi alifafanua kuwa kwa siku hospitali
hiyo, imekuwa ikipokea wagonjwa kuanzia 200 hadi 300 hivyo ni eneo ambalo
wadau wengine ikiwemo serikali ni lazima kuiongezea nguvu ya kifedha, watumishi
na vifaa tiba ili iweze kutoa huduma bora na za haraka.
No comments:
Post a Comment