Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAZIRI wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo,
amelitaka shirika la umeme Tanzania (TANESCO) hapa nchini, kubadili mwenendo
wake wa utendaji kazi, kwa kujenga mahusiano mazuri na wadau, mashirika ya watu
binafsi yenye mitambo ya kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji, ili kuweza
kupunguza tatizo la upatikanaji wa nishati hiyo muhimu.
Profesa Muhongo alitoa rai hiyo hivi karibuni,
alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma, akikagua na kutembelea
mitambo mbalimbali ya kuzalisha umeme pamoja na mgodi wa Ngaka unaozalisha
makaa ya mawe uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga
mkoani humo.
Uchimbaji wa makaa hayo ya mawe hufanywa na kampuni ya
Tancoal Energy ambapo Waziri huyo alipokuwa kwenye mgodi huo, alijionea kazi inayofanywa
na kampuni hiyo, huku akisisitiza kwamba hakuna sababu ya Watanzania kukosa
umeme kwa sababu makaa hayo yana uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 400 wenye
gharama nafuu, ambao utaunganishwa katika gridi ya taifa na kusambazwa katika
maeneo mbalimbali.
Aliagiza kwamba kampuni ya Tancoal Energy, kwa kushirikiana
na shirika la TANESCO wakae pamoja na kurekebisha bei za uzalishaji wa umeme,
ili mitambo ya uzalishaji wa nishati hiyo iweze kujengwa katika mgodi huo na
kuanza kazi ya uzalishaji ambao utaendana sambamba na soko lenye gharama nafuu.
“Naagiza TANESCO
jengeni ushirikiano na ondoeni kigugumizi, badala yake kuweni karibu na
makampuni haya binafsi ambayo yanauwezo wa kusambaza umeme kwa wananchi kwa bei
nafuu, ambayo kila mwananchi ataweza kunufaika nayo”, alisisitiza Profesa
Muhongo.
Aidha Waziri huyo alitembelea mitambo miwili ya kufua
umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ambayo ni wa Andoya Hydro Electric Power
(AHEPO) uliopo katika kijiji cha Lifakara wilayani Mbinga na ule ambao unamilikiwa
na shirika la Mtakatifu Benedict, Masista wa Chipole uliopo kijiji cha Tulila
Songea vijijini.
Mitambo hiyo hivi sasa inatoa huduma kwa wananchi, chini ya
shirika la TANESCO ambapo umeme umeunganishwa katika njia kuu na kuweza kuwafikia
wateja husika.
Kwa upande wake Meneja wa shirika hilo Kanda ya nyanda za juu
kusini, Joyce Ngahyoma alisema kuwa shirika hilo lipo tayari kushirikiana na mashirika binafsi yanayojishughulisha na uzalishaji wa umeme, hivyo kilichobaki
ni kukaa chini na kujenga makubaliano ya dhati namna ya kuboresha utoaji wa huduma
hiyo kwa jamii.
Kadhalika Meneja mauzo wa kampuni ya Tancoal Energy
inayochimba makaa ya mawe, Christopher Temba naye aliongeza kuwa makaa hayo
yamekuwa ni kati ya makaa bora Afrika na kwamba, mengi yanategemewa kuuzwa
kwenye viwanda vinavyozalisha saruji hapa nchini.
Temba alieleza kwamba katika kiwanda cha Dangote kilichopo
mkoani Mtwara, walikubaliana kitachukua tani 13,500 kwa mwezi, lakini hivi
sasa kimechukua tani 2,000 tu, jambo ambalo Waziri Muhongo aliutaka uongozi wa
kiwanda hicho kutimiza masharti ya mkataba walioingia na Tancoal, ikiwemo kutumia
mkaa wa hapa nyumbani na sio kuagiza nje ya nchi kama wanavyofanya sasa kwa
lengo la kukwepa kulipa ushuru na kodi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment