Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua tawi la benki ya Posta Songea mkoani Ruvuma. |
Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
TATIZO la kutokuwa na wafanyakazi wabunifu katika Benki ya
Posta Tanzania, imeelezwa kuwa ni moja kati ya changamoto ambayo ilichangia
kudorola kiuchumi na kuifanya benki hiyo, ishindwe kusonga mbele kimaendeleo katika
kuwahudumia wateja wake.
Aidha imefafanuliwa kuwa baada ya kubaini tatizo hilo, benki
hiyo imeunda utaratibu mwingine mpya ambao hivi sasa kasi yake ni kubwa ya
uendeshaji wa huduma za kibenki, na kufanikiwa kutengeneza faida ya shilingi
bilioni 10.3 katika miaka mitatu iliyopita.
Sabasaba Mushinge ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa benki ya
Posta hapa nchini, alisema hayo juzi katika hafla fupi ya uzinduzi wa tawi
jipya la benki ya Posta Songea mkoani Ruvuma, ambayo ilizinduliwa na Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Mushinge aalisema kuwa wameweza kufikia asilimia 70 ya
ukarabati wa matawi yote yaliyopo hapa nchini, na kwamba mafanikio hayo
yametokana na mabadiliko ya kiuongozi baada ya benki kwa muda mrefu kudorola
kiuchumi.
Alisema hivi sasa wanavikundi 30,000 vya wajasiriamali ambao
wamejiunga na benki wamepewa mikopo, ambayo huendesha shughuli zao mbalimbali
za kimaendeleo katika familia zao.
Vilevile hutoa huduma ya mikopo kwa wastaafu, ambapo jumla ya
wastaafu 21,000 hapa nchini wamepewa mkopo wa shilingi bilioni 41 na kwamba
wateja wake wameunganishwa na mfumo wa Sim banking, ambao hutoa huduma popote
pale walipo.
“Tumeweza pia kutumia shilingi milioni 150 kwa ajili ya kutoa
misaada ya ujenzi wa madarasa ya kusomea wanafunzi katika maeneo mbalimbali
hapa Tanzania na utengenezaji wa madawati ya kukalia watoto hawa, ombi langu
nawaomba watanzania wenzangu watumie huduma za kifedha katika benki yetu ili
waweze kuondokana na umaskini”, alisema Mushinge.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Majaliwa alipongeza jitihada
zinazofanywa na benki hiyo ya Posta hasa kwa kukuza mtaji wake wa ndani na
kuboresha matawi yake huku akisisitiza kwa kuwataka watendaji wake, kufanya
kazi kwa juhudi na maarifa ili banke hiyo iweze kusonga mbele.
“Wanaruvuma hii ni bahati kubwa kwenu, ni lazima sasa
tuonyeshe kwamba tunahitaji maendeleo makubwa kutoka katika benki hii, ili hawa
Posta waweze kufungua matawi mengi katika mkoa wetu”, alisema Waziri Mkuu
Majaliwa.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu Majaliwa aliutaka
uongozi wa benki ya Posta kuhakikisha kwamba inafungua milango kwa kutumia
matangazo ili elimu husika iweze kuwafikia wananchi kwa wakati, na kusisitiza
kuwa kutembea na fedha mifukoni kumepitwa na wakati hivyo Watanzania wanapaswa
kubadilika kwa kuwa na mazoea ya kuweka fedha benki.
No comments:
Post a Comment