Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MFANYABIASHARA mmoja ambaye anajulikana kwa jina la Elias Mwalewela
(46) anayeishi mtaa wa Manzese Mbinga mjini mkoani Ruvuma, amekamatwa akitorosha
kahawa ya maganda isiyokobolewa kiwandani, kwenda Jijini Mbeya kwa njia ya magendo
bila kufuata taratibu na sheria husika.
Aidha imeelezwa kuwa wakati zao hilo analitorosha, alikuwa
akitokea wilayani Mbinga mkoani humo kwa lengo la kuipeleka huko, huku akijua
fika kahawa ya maganda hairuhusiwi kusafirishwa kutoka wilaya moja kwenda
nyingine.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga,
Venance Mwamengo alisema kuwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema
juu ya utoroshaji huo, alichukua jukumu la kufuatilia suala hilo ndipo baadaye
alifanikiwa kumkamata katika kijiji cha Liganga wilaya ya Songea vijijini
mkoani hapa kwa kushirikiana na askari aliokuwa nao.
Alifafanua kuwa alimkamata Disemba 30 mwaka jana, majira ya
saa tano usiku akiwa na gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 818 ADH
ambalo lilikuwa likiendeshwa na Geati Mwajungwa mkazi wa Lujewa wilaya ya
Mbarali mkoani Mbeya.
“Huyu mfanyabiashara na dereva wake, baada ya kuwakamata
niliwafikisha kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga na gari lenye mzigo wa
kahawa tani nne ambalo linashikiliwa hapo kituoni, hivi sasa wanaendelea
kuhojiwa na taratibu zingine zitafuata ikiwemo kufikishwa Mahakamani au
wanapaswa kulipa faini ya shilingi milioni 20”, alisema Mwamengo.
Mwamengo aliongeza kuwa watoroshaji hao walipofika mpakani
mwa wilaya yake ambako kuna geti la ukaguzi wa mazao, walitorosha gari hilo likiwa
na kahawa hiyo ndipo jitihada zilifanyika za kuwasaka na kufanikiwa kuwakamata
katika kijiji hicho cha Liganga.
Alieleza kuwa wakati anawakamata, aliwakuta wakiwa na kibali
cha usafirishaji kahawa safi (Clean Coffee) ambacho ni cha kampuni ya Tutunze Kahawa
Limited, iliyopo wilayani humo ambayo inajishughulisha pia na ununuzi wa zao
hilo.
Vilevile aliongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu husika, kibali
hicho kinaruhusu kusafirishia kahawa iliyo safi tu, ambayo imekwisha kobolewa
kiwandani na sio ya maganda kama walivyofanya watu hao.
Kufuatia tukio hilo Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga naye
alithibitisha juu ya tukio hilo na kueleza kuwa mfanyabiashara huyo na dereva
wa gari hilo wanahojiwa na Jeshi la Polisi wilayani humo, ili waweze kutolea
maelezo ya kina juu ya kitendo hicho walichokifanya.
“Ni kweli taarifa nilizonazo wamekamatwa wakisafirisha kahawa
ya maganda (Mbuni) na wapo Polisi wanahojiwa, wakimaliza kuhojiwa nitakuwa na
taarifa kamili na kulitolea ufafanuzi mzuri jambo hili hapo baadaye”, alisema
Ngaga.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo alisema hataweza kutoa ufafanuzi
wowote kuhusiana na jambo hilo, akidai kwamba ofisi yake bado halijamfikia.
No comments:
Post a Comment