Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amemsimamisha kazi Meneja Shughuli
wa Kiwanda cha kusindika tumbaku mkoani Ruvuma (SONTOP) Paul Balegwa, na
kuvunja bodi ya kiwanda hicho, akidaiwa kushiriki kwa namna moja au nyingine
kufanya ubadhirifu wa fedha za wakulima wanaozalisha zao hilo na kusababisha
kiwanda hicho, kusitisha uzalishaji kwa zaidi ya miaka 18 iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano
wa Ikulu ndogo ya Songea, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa amefikia uamuzi wa
kumsimamisha kazi Meneja huyo kutokana na ubabaishaji mkubwa wa uendeshaji wa
kiwanda hicho ambao ulikuwa ukifanywa kwa kushirikiana na mhasibu wake Nurdin
Ponela, ambaye sasa inadaiwa amekimbia na kutokomea kusikojulikana.
Vilevile Waziri Mkuu huyo alifafanua kuwa wakulima wa zao la
tumbaku kwa muda mrefu wamekuwa wakiulalamikia uongozi wa kiwanda hicho kwamba,
viongozi wao kuwa ni wababaishaji huwakata fedha zao za mauzo ya tumbaku bila
kufuata utaratibu.
“Katika kiwanda hiki upo ubabaishaji mkubwa, wa uendeshaji wa
hata chama kikuu cha ushirika cha wakulima wa zao hili wilaya ya Songea na
Namtumbo (SONAMCU) kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa matumizi ya fedha na leo hii
natamka kwamba nimemsisha kazi Paul Balegwa na sheria zitafuata mkondo wake”,
alisema Waziri MKuu Majaliwa.
Kiwanda hicho ambacho kwa hivi sasa kimegeuzwa kuwa ghala la
kuhifadhia bidhaa mbalimbali za wafanyabiashara, hali hiyo ilimchukiza Waziri
Mkuu Majaliwa alipotembelea kwa kushitukiza na kujionea madudu hayo.
Kadhalika katika eneo la nje ya kiwanda hicho, imegeuzwa kuwa
sehemu ya kuegeshea magari yanayobeba makaa ya mawe kutoka mgodi wa Ngaka
ambayo yanachimbwa katika kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani humo.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu Majaliwa alimuagiza Mkuu
wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu akae na wataalamu wake akiwemo Afisa biashara
na uwekezaji wa Wizara ya viwanda na biashara Tanzania, Stella Lugongo kwamba
asiondoke mpaka watafute njia mbadala ya kuwatafuta wawekezaji ambao wataweza
kufufua kiwanda hicho, ambacho kilikuwa ni tegemeo kubwa kwa wakulima wanaozalisha
zao hilo mkoani humo.
Alisema kuwa ufufuaji wa kiwanda cha SONTOP utasaidia
kuongeza ajira kwa vijana zaidi ya 2,500 kama ilivyokuwa hapo awali, na kwamba
kikisha anza kufanya kazi itasaida pia kuongeza thamani ya zao la tumbaku na
kukuza uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Mapema Waziri Mkuu Majaliwa kufuatia kuwepo kwa tuhuma hizo,
alilazimika kumuagiza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Mwambungu ahakikishe kwamba kabla
hajamaliza ziara yake anahitaji kukutana na viongozi wa vyama vya msingi pamoja
na bodi ya kiwanda hicho ili aweze kupata taarifa kamili juu ya hali hiyo
ambayo ilisababisha kiwanda hicho kusimama.
Kwa nyakati tofauti baadhi ya wakulima pamoja na waliokuwa
wafanyakazi wa kiwanda hicho ambao hawakutaka majina yao yatajwe wameeleza kuwa
kiwanda cha kusindika tumbaku cha SONTOP kilichopo katika Manispaa ya Songea,
kilisimama kusindika zao hilo kufuatia kuingiwa kwa mikataba mibovu kwa baadhi
ya viongozi iliyoambatana na ubadhirifu wa fedha ambao ulisababisha kiwanda
kishindwe kujiendesha.
Walisema kuwa katika mikataba hiyo, ina makampuni yanayonunua
zao hilo, iliweka masharti ya kusindika tumbaku kwa kutumia viwanda vilivyoko
mkoani Morogoro jambo ambalo lilisababisha kupoteza ajira za vijana wengi waliokuwa
wakifanya kazi.
Hata hivyo Waziri Mkuu Majaliwa amemaliza ziara yake ya siku
tatu mkoani Ruvuma, na kuondoka kurejea Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
kutekeleza majukumu mengine ya kazi za kitaifa.
No comments:
Post a Comment